Home Uncategorized SERIKALI YAZUIA MASHABIKI WA SIMBA KUSHEREKEA UBINGWA

SERIKALI YAZUIA MASHABIKI WA SIMBA KUSHEREKEA UBINGWA

Serikali imepiga marufuku mashabiki wa soka katika mikoa nje ya Dar es Salaam, kuingia viwanjani kutazama mechi za Ligi Kuu zitakazohusisha timu za Simba na Yanga kuanzia leo hadi pale itakapojiridhisha.

Agizo hilo limetolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufuatia kukiukwa kwa miongozo iliyowekwa ya kukabiliana na virusi vya Corona vnavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika jana katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, baina ya Mbeya City na Simba.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo jioni, serikali imesema imechukua hatua hiyo baada ya kubaini kutofuatwa kwa miongozo iliyowekwa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na virusi hivyo.

“Wizara inaelekeza kuwa kuanzia leo mechi zote zitakazohusisha timu za Simba na Yanga nje ya Dar es Salaam, mashabiki hawataruhusiwa kuingia uwanjani kuangalia mechi zilizosalia.

Isipokuwa tu pale itakapojiridhisha kupitia kamati za ulinzi na usalama za mikoa husika ya klabu mwenyeji na mgeni ambao watalazimika kuwasilisha kwa maandishi mpango mkakati wao, iwapo mashabiki wataruhusiwa kuingia ili kuzuia watu kujazana uwanjani. Mpango huo uwasilishwe Baraza la Michezo la Taifa (BMT),” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara, timu mwenyeji ambayo ilikuwa ni Mbeya City na wasimamizi wa mchezo huo, walishindwa kusimamia utekelezaji wa miongozo ya kupambana na virusi vya Corona, jambo lililopelekea ichukue uamuzi huo mzito.

“Serikali imezuia timu ya Mbeya City ya Mbeya kucheza na mashabiki kwa mechi zake zote zilizosalia kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine jijini Mbeya kutokana na na kukiukwa kwa mwongozo wa afya michezoni wakati wa mchezo kati ya timu hiyo na klabu ya Simba ya Dar es Salaam,” ilifafanua taarifa hiyo ya Wizara.

Wiki iliyopita, serikali iliipa adhabu timu ya JKT Tanzania ya kucheza mechi zake za nyumbani bila mashabiki baada ya ukiukwaji wa miongozo ya kujikinga na virusi vya Corona iliyowekwa na serikali.

SOMA NA HII  KOCHA POLISI TANZANIA AFICHUA KILICHO NYUMA YA KUSHINDWA MBELE YA SIMBA