Home Uncategorized ANGALIA SIMBA ILIVYOBEBA KWA UBINGWA WA GD TU, JIFUNZE…

ANGALIA SIMBA ILIVYOBEBA KWA UBINGWA WA GD TU, JIFUNZE…


Na SALEH ALLY
SIMBA amekuwa bingwa tangu juzi Jumamosi ingawa wengi hawakuwa wameling’amua hili mapema kwa kuwa walisubiri kuiona ikicheza mechi yake ya jana dhidi ya Prisons ya Mbeya.


Kikosi cha Simba kilikuwa jijini Mbeya kikisubiri mechi hiyo ili kutangaza ubingwa rasmi kwa kuwa awali ilihitajika pointi tatu tu kumaliza kazi.


Hii ilikuwa imeaminika hivyo, kiuhalisia, Simba ilihitaji pointi moja tu kutoka Mbeya baada ya mechi za jana lakini hata bila ya hiyo pointi moja, tayari ilishakuwa bingwa.


Mambo yalikuwa hivi, hapa tunaweza kujifunza umuhimu wa mabao ya kufunga na kufungwa katika mchezo wa soka na namna Simba ilivyokuwa bingwa kupitia Goal Difference (GD).


Nimesema Simba ilikuwa bingwa tangu juzi Jumamosi na ilichukua ubingwa kupitia GD ikiwa ni mara ya Azam FC kutoka sare ya mabao 1-1 dhidi ya Biashara United na Yanga wakashinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Ndanda FC.


Angalia, baada ya sare ya Azam FC na Biashara, Azam FC ikafikisha mechi 32 na pointi 59, baada ya ushindi dhidi ya Ndanda FC, Yanga ikawa na pointi 60 na michezo ikawa 32 pia.


Michezo iliyobaki kwa Azam FC na Yanga, kila moja ni sita. Iwapo Azam FC ikishinda mechi zake zote itafikisha pointi 77, tayari Simba imeshafikisha pointi 78 ikiwa na mechi 31.


Iwapo Yanga itashinda mechi zake sita zilizobaki, itafikisha pointi 78. Sawa kabisa na zile ambazo tayari Simba wamekusanya wakiwa na mechi 31.


Wengi hawakuwa wameling’amua hilo, nikawasikia baadhi ya wanaozungumzia mpira kuwa ilibaki pointi moja tu Simba iwe bingwa. Lakini uhalisia, wingi au ukubwa wa GD na tofauti ya GD kati ya yake na Yanga na Azam FC, uliamua Simba kuwa bingwa ikiwa mkononi na mechi saba.


Kwa nini Simba kawa bingwa, hapa ndipo tunakwenda kujifunza katika GD. Kwamba ina umuhimu wa juu sana katika suala la baadaye na inapaswa kuipa nafasi kubwa wakati wa mechi za mapema maana kuna wakati inaweza kuwa msaada huko mbeleni.


Kwa Simba, imeisaidia kubeba ubingwa ikiwa na mechi 31 tu, ingawa wengi walitaka kusubiri hadi iongezeke angalau pointi moja ili waseme uhakika.


GD ya Azam FC baada ya mechi 32 ni 18, hawa tayari walishaondoka katika vita ya kuipunguzia Simba kasi ya kubeba ubingwa mapema na hasa baada ya sare dhidi ya Biashara ya Mara.


Angalia GD ya Yanga ni 13, Simba wana GD ya 53. Zaidi ya mara nne ya waliyonayo Yanga. Kama zimebaki mechi sita, Yanga wanaweza kutengeneza mabao 40 bila ya kufungwa hata moja?


Tena walikuwa wanatakiwa kutengeneza mabao 41 ndani ya mechi zita bila ya kufungwa hata moja ili waweze kuipiku Simba katika suala la ubingwa.


Unaona, Simba mwanzo imeshinda ubingwa wa Tanzania Bara kwa tofauti hiyo ya mabao ya kufunga na kufungwa, GD.


Funzo hapa ni kwamba timu zinapaswa kujipanga mapema katika suala la kufunga mabao mengi na kuzuia kwa uhakika au kufungwa mabao machache zaidi.


Simba imebeba ubingwa kwa uhakika sana kwa kuwa ilicheza mechi zake kwa umakini sana, ikafungwa mabao machache na kufunga mengi hivyo kutengeneza GD bora.


Kutengeneza GD bora ni kufunga mabao mengi na kufungwa machache. Katika msimu huu, ndani ya mechi 31, tayari Simba ilishafunga mabao 69 na kufungwa 13 tu.


Hii maana yake hivi, Simba imekuwa na timu bora zaidi maradufu ya nyingine unapozungumzia mabao ya kufunga katika ligi hiyo lakini ikawa na difensi bora zaidi, hapa ni ulinzi.


Unafanyaje kuwa na safu bora ya ushambulizi na ulinzi, tunajua kwanza ni wachezaji sahihi na pili kocha wa uhakika na maandalizi ya uhakika. Katika hili viongozi wanakuwa wanahusika zaidi na baada ya hapo ni wachezaji na benchi la ufundi.


Hongereni Simba kwa kubeba ubingwa mkitoa funzo, huenda kwa watakaolichukulia kama funzo wanaweza kujifunza mechi kupitia msimu huu ambao mmebeba ubingwa mkiwa “mnakunywa kahawa” pale mjini Mbeya.

SOMA NA HII  BOB HAISA AREJEA NA PENZI LA KARAHA