Home Uncategorized KUHUSU YANGA..BOCCO AMGOMEA BOSS WA GSM..!!!

KUHUSU YANGA..BOCCO AMGOMEA BOSS WA GSM..!!!

NAHODHA wa Simba, John Bocco, amemgomea Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, juu ya tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Wakati Mhandisi Said akiamini Yanga itatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kujinyakulia tiketi ya kushiriki michuano hiyo ya Afrika, Bocco amekataa kata kata akisema Wanajangwani hao ni kama wanaota ndoto ya mchana.

Alichosema Bocco ni kwamba pamoja na timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na hivyo kujihakikishia kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, bado wanatamani taji la ASFC.

Tambo hizo za Bocco zinamaanisha kuwa iwapo Simba watakomaa na kushinda mchezo wao wa robo fainali ya ASFC kesho dhidi ya Azam, Mhandisi Said na Yanga yake, wasitarajie kufika fainali kwani wataikatiza safari yao katika michuano hiyo watakapokutana nao nusu fainali.

Iwapo Yanga itaichapa Kagera Sugar leo katika robo fainali ya kwanza ya ASFC, itakutana na mshindi kati ya Azam na Simba, hivyo kama akina Bocco watavuka, watemenyana na watani wao hao wa jadi nusu fainali.

Akizungumza na gazeti la  BINGWA jana, jijini Dar es Salaam, Bocco alisema baada ya kutwaa ubingwa wa Bara, kilichopo mbele yao ni kubeba kombe la ASFC, hivyo kutimiza azma yao ya kutoacha kitu msimu huu.

“Haya ni mafanikio makubwa kwangu na jambo la kukumbukwa sana, najivunia kuwa kiongozi katika timu na kuiwezesha kuchukua ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo, sasa kilichopo mbele yetu ni kombe la FA.

“Nawaahidi wanachama na mashabiki kuwa nikiwa ndani ya timu hii, tutaendelea kuchukua ubingwa, bado tuna miaka miwili ijayo ambayo taji litakuwa letu na hata kombe la FA tutalichukua tu kwani tupo fiti na kila mmoja anatamani kuona tunachukua makombe yote mawili,” alisema Bocco.

Hivi karibuni, Mhandisi Said aliwahi kuliambia gazeti la BINGWA kuwa baada ya kuelekea kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, watafanya kila wanaloweza kuhakikisha wanabeba kombe la ASFC ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

SOMA NA HII  ANALIPWA BIL 2 KWA TANGAZO MOJA