NGOMA ikipigwa sana mwisho wake hupasuka hivyo katika kila jambo ambalo unalifanya kwa sasa ni lazima kuwa na kiasi ili uweza kuwa na usawa bila kujali upepo unakwendaje.
Nimeamua kuanza hivyo baada ya kuona kwamba upepo umebadilika ghafla kwa wachezaji wengi ambao wanapewa sifa kubwa kwa kuwa wanafanya makubwa ndani ya uwanja wanashindwa kulinda thamani yao.
Muhimu kwa kila mchezaji anapaswa kufanya mambo makubwa matatu, jambo la kwanza ni kuwa na nidhamu, jambo la pili kuwa na nidhamu na jambo la tatu ni kuwa na nidhamu kazi itakuwa imeisha.
Ikiwa mchezaji anaweza kuwa na nidhamu katika kila anachokifanya inakuwa rahisi kwake kufanikiwa kwani ikiwa hauna nidhamu hata ukiwa na kipaji hilo ni sawa na hamna kitu kabisa.
Pili ukiwa na nidhamu ni rahisi kukubalika kila sehemu utakayokwenda hivyo kama utakosa nidhamu inakuwa ngumu kwa mchezaji kukubakika pale anapokwenda kwa viongozi hata wachezaji pia inakuwa ni ngumu.
Tatu, ukiwa na nidhamu inakujengea hali ya kuaminika na kila mmoja ambaye anaishi na wewe na inakuwa rahisi kuweza kupata msaada na wakati mwingine hata kuwa na marafiki wengi wazuri ambao watakuwa msaada hapo kesho kwani kila siku ni muhimu kutazama yale uliyofanya jana.
Nimeanza hivyo ili kuwakumbusha wale ambao ni wachezaji na wanadhani watakuwa kwenye mpira maisha yote hapana, zama zinapita na muda pia utameguka vilevile.
Kama ambavyo janga la Corona lilikuwa ni hofu kwa dunia nzima hatimaye taratibu linazidi kupungua huku Mungu akizidi kutulinda watu wake.
Katika hili ni muhimu kwa kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari binafsi na kuwalinda wengine ambao wamejisahau wakidhani kwamba Corona imeisha hapana bado ipo na Serikali inasisitiza kwamba ni lazima tahadhari zichukuliwe.
Narudi sasa kwenye mada ya leo hapa nitaanza kuzungumzia kwanza Ligi Daraja la Kwanza kwa kweli hapa ni lazima niweke wazi kwamba kundi A lina balaa kubwa na zito ambalo isipotazamwa kwa jicho la kipekee kuna mchezo mchafu utachezwa.
Kwa upande wa kundi B, Gwambina wale pale washakaa pembeni wanasoma magazeti ya kile ambacho kiliandikwa kuhusu wao wakati wanashiriki Ligi Daraja la Kwanza ila hapa sasa kundi A ninarudia tena kundi A ni moto lazima litazamwe kwa umakini.
Mechi zilizochezwa ni 20 kwa kila timu na kila timu imepata kile inachostahili katika hili timu zote zinapaswa hongera na pongezi pia kwa kuwa zinaonyesha zina uhitaji mkubwa.
Pia sijasahau kuwapa pongezi Gwambina neno langu ni moja tu kwenu kuweni na nidhamu huku ndani ya Ligi Kuu Bara mambo ni magumu ila hayatishi inawezekana.
Kisha baada ya kuwapa pongezi Gwambina ndugu zetu ambao wanauhakika na maisha mapya wakiwa wanatamba na mechi mbili mkononi pamoja na Uwanja wao wa Gwambina Complex basi tunarejea kwenye mada yetu.
Hapa ninazungumzia kundi A ambalo vita kubwa imebaki kwa Dodoma Jiji FC na Ihefu FC kwenye kupanda Daraja kabla ya kufikiria kucheza play off.
Ninataka kuachana na play off kwa kuwa hiyo haina matatizo mshindi wa pili na wa tatu hawa watamenyana na washindi wale wa kundi B ili kuwapata washindi wawili ambao watakipiga na wale wawili ambao wanatafutwa ndani ya Ligi Kuu Bara.
Hesabu za Dodoma FC ni kupanda ligi na Ihefu pia wanawaza hichohicho ni patamu kweli balaa na inafurahisha hasa kwa namna ambavyo wanapata matokeo.
Wote wakiwa wamecheza mechi 20 kibindoni wana pointi 45 jambo ambalo linaongeza ushindani katika kazi ya kusaka nafasi ya kufikia malengo ambayo wamejiwekea.
Kikubwa ni kuona kwamba kila timu inapata matokeo kwani hakuna ambaye hajui figisu ambazo huwa zinafanyika hivyo umakini mkubwa unatakiwa ili kufikia malengo ya kila mmoja bila kuharibu mipango ya mwingine.
Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) kwenye mechi hizi mbili ambazo hawa washindani wawili wanacheza inahitajika umakini mkubwa ili kila mmoja asipate sehemu ya kulalamikia pale ambapo mambo yatakwenda kombo.
Ukweli ni kwamba kila timu inahitaji kupata pointi tatu kwenye mechi ambazo wanazisaka hasa kuanzia kwenye mechi zao ambazo wanazicheza leo.
Ihefu na Dodoma tofauti yao ni mabao ya kufungana ambapo Dodoma ina mabao 33 na Ihefu ina mabao 28 hapa unaona picha ilivyo utashangaa mambo yanatokea hapo timu moja inashinda mabao 10 kwenye mechi moja hii haitapendeza kutokea.
Tazama na mechi ambazo wameshinda wote wameshinda 14 sare wote wanazo tatu na ukigusa zile za kufungwa wote ni tatu hivyo wana pacha matata kweli.
Ninachokiona mimi ni kwamba kwa kuwa ushindani ni mkubwa kwenye mechi za hawa washindani ni lazima kuwe na uangalizi mkubwa katika kufuatilia na kutazama namna gani mechi zitachezwa.
Ikiwa kutakuwa na ushirikiano mkubwa kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake zile ishu za upangaji matokeo hazitakuwepo na nina amini kwamba kutakuwa na usawa na mshindi atapatikana kwa haki.
Kila timu inahitaji kupanda na kushiriki ligi ila ni namna gani itaweza kufikia huko inakohitaji muhimu kuwe na mipango sahihi na ufuatiliaji makini wa matukio.
Viongozi wa timu husika ni lazima kuzingatia kwamba muhimu kuwa na maandalizi mazuri ili kufikia malengo ambayo wamejiwekea kila kitu ni rahisi iwapo utafanya mambo matatu katika maisha basi kazi itakuwa imwekwisha.