IMEELEZWA kuwa, uongozi wa Azam FC upo mbioni kumshusha Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola ili kuongeza nguvu kwenye benchi lao la ufundi.
Matola ni kocha msaidizi ndani ya Simba akiwa chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck ambao ni mabingwa wa taji la Ligi Kuu Bara, 2019/20.
Azam ambayo imetwaa Kombe la Ligi Kuu Bara mara moja tu tangu ipande daraja mwaka 2008, imejikuta ikiangukia pua msimu huu baada ya mipango yao kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na FA kuvurugika.
Taarifa ambazo Spoti Xtra imezipaa kutoka viunga vya Azam FC, zinaeleza kuwa, uongozi wa klabu hiyo upo katika mchakato wa kuboresha benchi lao la ufundi kwa kumleta Matola baada ya kubaini uwezo wake ni wa kiwango cha juu.
“Azam inahitaji kufanya maboresho katika benchi lake la ufundi kwa kumleta kocha Matola ambaye ameonekana ka kiwango kizuri ili aweze kuja kuibeba timu ambayo inaonekana kuwa na mwendo wa kupanda na kushuka kila msimu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Baada ya taarifa hizo kufika kwenye Dawati la Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema: “Kwa sasa tuna kocha msaidizi, lakini kama litakuwa ni pendekezo la mwalimu iwapo atahitaji msaidizi yeyote atapewa.
“Sijapata hiyo taarifa kuhusu Matola kutakiwa hapa, lakini watu waelewe kwamba tunamuheshimu Matola kwa sababu aliwahi kuwa mchezaji wetu wakati timu ilivyokuwa ikipanda daraja.”
Alipotafutwa Matola mwenyewe kuhusiana na ishu hiyo, kwanza alionekana kushtuka kisha akasema: “Hiyo taarifa bado haijanifikia, hivyo siwezi kuzungumzia kitu chochote kwa sasa, lakini ikinifikia na kuwa rasmi, nitazungumza.”