HATUA moja ambayo inapigwa katika maisha ya kila siku ni mwanzo wa mafanikio na anguko pia ambalo ni ishara kwamba kuna sehemu mambo hayakuwa sawa hivyo ni muhimu kujipanga.
Kwa sasa kazi ya kupambania nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Bara inakwenda kumalizwa rasmi Julai 11 ambapo mechi zitakazochezwa zitahitimisha enzi ya ubabe na safari ndefu ya mechi 22 kwa kila timu.
Haikuwa kazi rahisi ila mwisho wa siku inakwenda kuhitimishwa ili kuruhusu maisha kuendelea wakati ujao kwa msimu wa 2020/21.
mtifuano ulivyo kwenye kupanda na kushuka kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza namna hii:-
Kazi yao imeisha
Gwambina FC imeshamaliza kazi kwenye Kundi B ambapo tayari ina uhakika wa kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Wanasaka nafasi ya playoff
Kuna nafasi ya kucheza playoff kwa timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ambapo mshindi wa pili Kundi A atacheza dhidi ya mshindi wa tatu Kundi B, na mshindi wa pili Kundi B atacheza dhidi ya mshindi wa tatu Kundi A.
Washindi wa jumla wa mechi hizi watakutana na timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ambazo zitamaliza kwenye nafasi ya 15 na 16.
Kwenye Kundi A, hivi sasa vinara ni Dodoma FC ambao wapo sawa kwa pointi na Ihefu SC, tofauti yao ni mabao ya kufunga na kufungwa tu. Mechi ya mwisho wikiendi hii ndiyo itaamua nani anapanda daraja moja kwa moja kutoka Kundi A. Zote zina pointi 48.
Nafasi ya tatu katika kundi hili inakamatwa na Majimaji ambayo inahitaji pointi moja tu kujihakikishia nafasi hiyo ili icheze play off ya kupanda daraja.
Kundi B patamu
Geita Gold wana uhakika wa kucheza play off kwa kuwa wana pointi 34 kibindoni. Gipco ipo nafasi ya tatu na Transit Camp nafasi ya nne zote zina pointi 30 pamoja na Rhino Rangers yenye pointi 29 iliyo nafasi ya tano zote zikiwa zimecheza mechi 21, zinawania nafasi moja ya kucheza play off, hivyo dakika tisini zitaamua nani ni nani.
Hawa hapa wanaporomoka
Timu nne zinashuka hadi Ligi Daraja la Pili. Kwa Kundi A mambo yapo namna hii:-
Mlale FC ipo nafasi ya 12 ina pointi 11, Pan African ipo nafasi ya 11 na pointi zake 17, Cosmopolitan ipo nafasi ya 10 ina pointi 19. Hizi zote zimecheza mechi 21 tayari muda wao umeisha na zinashuka jumlajumla.
Iringa United iliyo nafasi ya 9 na Friends Rangers iliyo nafasi ya 8 zote zina pointi 24 mchezo wa mwisho utaamua nani abaki nani ashuke.
Kundi B wanakwenda na maji hawa hapa:-
Green Warriors tayari safari yao ishaisha ambapo wapo nafasi ya 12 na pointi 21 baada ya kucheza mechi 21.
Sahare All Stars ipo nafasi ya 11 na pointi 23, Stand United ipo nafasi ya 10 na pointi 24, Mawenzi FC ipo nafasi ya tisa na pointi 24 zote zimecheza mechi 21.
Ili kuaga rasmi ndani ya Ligi Daraja la Kwanza matokeo yao ya mwisho yataamua nani ashuke jumlajumla kwenye mechi zao watakazocheza.
Hizi hapa zimeshikilia ushindi
Mechi mbili za mwisho ambazo zitakuwa na mvuto wa aina yake ni ile ya Dodoma FC vs Iringa United na Ihefu SC vs Cosmopolitan.
Utamu wa mechi hizo unakuja kutokana na Dodoma na Ihefu kuwa pointi sawa kileleni mwa Kundi A, huku Iringa United nayo inataka kujinasua na janga la kushuka daraja.
Dodoma FC iliyo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 48 kwenye msimamo itamenyana na Iringa United iliyo nafasi ya 9 na pointi 24 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ihefu iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 48, itamenyana na Cosmopolitan iliyo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 22 ikiwa tayari imeshashuka daraja. Mechi hii itapigwa Uwanja wa Highlands Estates, Mbarali, Mbeya.