UONGOZI wa Yanga umesema kuwa kiungo wao Mghana, Bernard Morrison asitegemee wao kutangaza kuvunja mkataba wake huku wakisisitiza kuwa mchezaji huyo bado ni mali yao mwenye mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kukipiga Jangwani.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Mghana huyo kuondoka uwanjani wakati timu hiyo ikiendelea na mchezo wake wa Nusu Fainali ya Kombe la FA walipocheza na Simba na kulala kwa mabao 4-1, baada ya kutolewe katika dakika ya 64.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela,amesema kuwa kiungo huyo bado ni mali yao hadi Julai 15, 2022, baada ya kuongeza mkataba wake wa miaka miwili.
Mwakalebela alisema kuwa kiungo huyo kama anafanya matukio ya kiutovu wa nidhamu kwa makusudi akitegemea uongozi utasitisha mkataba wake na kuondoka kama mchezaji huru, basi imekula kwake.
Aliongeza kuwa kiungo huyo ataondoka kwenye timu hiyo mara baada ya mkataba wake kumalizika huku ukimtaka kutumia njia nzuri na sahihi ya kutaka kuondoka kwenye timu na siyo kufanya vituko.
“Sisi Yanga wala hatuna shida na Morrison, kikubwa kama anataka kuondoka ni vema akatumia njia zilizokuwa sahihi na siyo kufanya vituko akiamini sisi tutatangaza kuachana naye.
“Hivyo basi anatakiwa kufahamu kuwa yeye ni mchezaji halali wa Yanga mwenye mkataba wa miaka miwili.
“Hatutakuwa tayari kuachana naye hadi pale timu itakayomhitaji kutufuata kukaa meza moja kufikia makubaliano mazuri ya kuuvunja mkataba wake wa miaka miwili,” alisema Mwakalebela.
Chanzo: Championi