MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wameshindikana kwenye mechi zao tatu ambazo ni dakika 270 walizocheza Uwanja wa Taifa kwa kufunga idadi kubwa ya mabao ambayo haijafikiwa na watani zao Yanga huku wachezaji wawili, Luis Miqussone na Meddie Kagere wakiwapoteza wale wa Yanga.
Simba na Yanga zikiwa Dar, zimecheza mechi tatu za ushindani ikiwa ni mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho, hatua ya nusu fainali na mechi mbili za Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hizo tatu, Simba imefunga jumla ya mabao 11 huku Yanga ikifunga jumla ya mabao matano, Kwa upande wa mabao ya kufungwa Simba imefungwa mabao matano huku Yanga ikifungwa mabao sita.
Mechi zao zilikuwa namna hii:- Julai 12, Simba 4-1 Yanga,Julai 16, Simba 2-3 Mbao na Julai 16, Simba 5-1 Alliance FC. Kwa Yanga ilikuwa Julai 12, Simba 4-1Yanga,Julai 15, Yanga 3-1 Singida United na Julai 18, Yanga 1-1 Mwadui FC.
Mbali na idadi ya mabao ya kufunga kwa upande wa Simba kuipoteza Yanga, pia ndani ya dakika 270, washambuliaji wa Simba wamekuwa na kasi ya kucheka na nyavu mfululizo.
Meddie Kagere mtupiaji namba moja ameweka rekodi ya kufunga mabao matatu mfululizo huku akifunga mabao mawili kwa penalti kwa guu lake la kulia na mabao yote matatu akifunga lango la Kusini kwa guu la kulia.
Aliibuka mbele ya Mbao wakati Simba ikilala kwa mabao 2-3 kwa penalti kisha akaibuka mbele ya Alliance, wakati Simba ikishinda mabao 5-1.
Kwenye mabao hayo 11, Kagere na Luis Miqussone wamekuwa ni moto wa kuotea mbali ambapo wamehusika kwenye jumla ya mabao 8, Kagere amefunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao huku Luis akifunga mabao mawili, pasi moja ya bao na alisababisha penalti moja iliyofungwa na Kagere kwenye mchezo wa Alliance.
Kwa upande wa Yanga, Feisal Salum na Mrisho Ngassa wamehusika kwenye jumla ya mabao manne kati ya matano, ambapo Fei Toto amefunga mabao mawili huku Ngassa akifunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao.