MATUMAINI ya Yanga na Azam FC kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, huenda yakatimia endapo kauli ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuiondoa Libya katika nchi ambazo zinatoa timu nne kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa itatolewa rasmi.
Yanga na Azam wanaweza kupata nafasi hiyo ya kwenda kimataifa msimu ujao kama watafanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili na ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu, ambapo wataungana na bingwa wa nchi Simba na Namungo katika kuiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo makubwa.
Kupitia michuano inayoendelea msimu huu, Libya iliweza kuipiku Tanzania miongoni mwa nchi zenye sifa ya kutoa timu nne kwenye michuano hiyo baada ya kufikisha alama 16.5, wakati Tanzania ikishika nafasi ya 13 ikiwa na alama 14 kutokana na Yanga, Simba na Azam kushindwa kung’ara kimataifa.
Kwa mujibu wa mtandao wa Libyan Express, Caf wameshaiondoa Libya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020/21 kutokana na kushindwa kumalizika ligi na hata walipoisitisha haikuwa imechezwa kwa asilimia 50.
Hata hivyo, kulingana na kanuni za Caf nchi ambayo haitaendesha ligi yake kwa angalau msimu mmoja inapoteza nafasi zake zote na kuchukuliwa na nchi ambayo ilikuwa inafuatia kwa chini yake.
Hivyo Libya wao ligi yao ilisimama kutokana na uwepo wa Virusi vya Corona.Aidha nchi za Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati nazo zimetangaza kujiondoa kushiriki michuano hiyo msimu ujao kutokana na janga la Virusi vya Corona na hivyo kuongeza matumaini ya Tanzania kurudishiwa nafasi zake nne kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.
Kama hili litatokea, klabu za Yanga na Azam FC zitaungana na Simba na Namungo FC ambazo tayari zimekata tiketi.
Timu itakayomaliza nafasi ya pili itacheza Ligi ya Mabingwa sawa na Simba wakati ile itakayomaliza nafasi ya tatu itacheza Kombe la Shirikisho sawa na Namungo.
Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliwahi kunukuliwa akisema: “Bado hatujapokea taarifa rasmi kutoka Caf ingawa ni kweli kuwa taarifa ya Libya kuondolewa kwenye michuano hiyo tumeziona mtandaoni kama ninyi na zinazungumzwa katika vyanzo vingi vya habari Afrika. Kwa hiyo tuwe na subira.”
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam FC, ambao na wenyewe wanaweza wakapata bahati hiyo, Thabit Zakaria (Zaka Zakazi), aliliambia Championi kuwa: “Unajua sisi tunahitaji zaidi kushika nafasi ya pili, kwa sababu kuna uwezekano Libya wakaondolewa kucheza klabu bingwa, hivyo nchi ambayo itachukua nafasi hiyo ni Tanzania na ikiwa hivyo zitakwenda timu nne na sisi tukiwepo kama tukishika nafasi ya pili.”