BEKI wa kushoto wa kimataifa wa Rwanda anayeichezea Rayon Sports, Eric Rutanga ni mali ya Yanga baada ya kusema kuwa ameshasaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.
Hivi karibuni Yanga kupitia kwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said alisema kuwa baadhi ya wachezaji wataanza kuwasili nchini hivi karibuni baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, ishara inayoonyesha kuwa Rutanga atatua nchini siku chache zijazo.
Rutanga amesema kuwa tayari ameshamalizana na Yanga baada ya kukubali kusaini mkataba wa miaka miwili ambapo alisema kuwa iliwabidi Yanga wamtumie mkataba kwa njia ya mtandao ‘Email’ kwa kuwa mipaka ya Rwanda haijafunguliwa.
“Namshukuru Mungu kila kitu kimeenda sawa kama ambavyo nilikuwa nikitarajia, tayari tumeshamalizana na Yanga na nimesaini mkataba wa kuitumikia kwa miaka miwili, hivyo uongozi wa Yanga umeniambia nisubiri mipaka itakapofunguliwa ya Rwanda watanitumia tiketi ya ndege.
“Hapo awali nilikuwa na mashaka kwa kuwa mipaka ilikuwa imefungwa hivyo kukamilika kwa dili langu ilikuwa ni ngumu ndiyo viongozi wa Yanga waliponitumia mkataba kupitia Email na mimi ikanibidi nisaini kisha nikatumia tena Email kuwajibu, hivyo hivi karibuni nitakuja Tanzania,” alisema beki huyo ambaye alijiunga na Rayon akitokea APR.