MFALME wa Bongo Fleva, Alikiba amefunguka kuwa Team Kiba hawatakubali tena kufungwa na Team Samatta katika mtanange wa hisani wa SamaKiba Foundation ambao unakwenda kupigwa Uwanja wa Taifa Dar, Agosti 8, mwaka huu.
Kiba amesema walikuwa na bahati mbaya katika misimu miwili iliyopita na kujikuta wakifungwa katika mechi zote mbili, licha ya kuwa kikosi chao kilikuwa bora zaidi ya kile cha Team Samatta, hivyo awamu hii ni ni zamu yao kuwapa raha mashabiki wa TeamKiba.
Mchezo huo wa SamaKiba Foundation ulianzishwa kwa kuunganisha nguvu kati ya nyota wa Aston Villa ya England, Mbwana Samatta na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba kwa lengo la kukusanya fedha na kuzisaidia jamii za watu wa hali ya chini.
Akizungumza na Championi Jumatano, Alikiba alisema: “Haiwezekani tufungwe mara tatu mfululizo, hiyo ngumu kutokea msimu huu, awamu hii ni zamu ya TeamKiba kushinda, hatutakubali kufungwa tena kizembe, kwanza sisi tunakuwa na bahati mbaya tu, kama kwa kikosi sisi huwa ni bora kuliko wao.”
Mbwana Samatta tayari ameshatangaza timu ya watu watano ambao ni Mohamed Samatta, Idd Seleman ‘Nado’, Farid Mussa na Juma Kaseja na msemaji wake ni Haji Manara, ambaye ni Ofisa Habari wa Klabu ya Simba.
Kwa upande wa Kiba yeye kamtaja Juma Mgunda kuwa kocha wake na Mwalubadu kuwa msemaji.
Huku wasanii wake wawili wa Kings Music, K2ga na mdogo wake Abdu Kiba wakitajwa kuwa sehemu ya kikosi hicho. Matokeo yaliyopita yalikuwa hivi, msimu wa kwanza ambao ulikuwa ni Juni Mosi, 2018, Team Samatta 3-1 TeamKiba, huku msimu wa pili uliofanyika Juni 11, Team Kiba walifungwa 6-3.