MKURUGENZI Uwekezaji wa GSM na Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hersi Said, ametaja majukumu atakayoyafanya aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Senzo asaini mkataba wa kufanyakazi na Yanga mara baada ya kuachana na Simba.
Hersi ameliambia Spoti Xtra kuwa, Senzo ametua hapo kusaidia kusimamia mabadiliko ya utawala ndani ya klabu hiyo na siyo kuwa mtendaji mkuu.
Aliongeza kuwa, ni ngumu kwa Senzo kuwa mtendaji mkuu wa Yanga kutokana na katiba kutoruhusu kiongozi wa kigeni kufanya majukumu hayo makubwa.
Yanga hivi sasa ipo kwenye mchakato wa mwisho wa kukamilisha mfumo wa mabadiliko wa uongozi ambapo hivi karibuni waliingia makubaliano na La Liga waliopewa jukumu la kusimamia zoezi hilo.
“Senzo anakuja kusimama katika kusaidiana na uongozi kwenye mabadiliko ya utawala ambayo tayari ungozi wameuanza kwa kushirikiana na GSM ambao ndiyo wanaosimamia kufanikisha zoezi hilo.
“Kwa hivi sasa hawezi kuwa ofisa mtendaji mkuu kwa kuwa katiba ya klabu hairuhusu kiongozi kama huyo raia wa kigeni kuja kupewa jukumu hilo.
“Mara baada ya mchakato huu wa mfumo wa mabadiliko wa uongozi wa Yanga utakapokamilika ndiyo anaweza akachukua nafasi hiyo ya utendaji,” alisema Hersi Said.
Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa Senzo Jumatatu jioni alienda Simba na kukabidhi ofisi na vifaa vyote vya klabu hiyo ikiwemo gari aina ya 2020 Mercedes-Benz alilopewa na mwekezaji wa klabu hiyo, bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Wakati huohuo, uongozi wa Simba umesema itakuwa ngumu hivi sasa Senzo kuanza kazi ndani ya Yanga kwa kuwa kibali chake cha kazi kinamtambulisha kuwa ni mali ya Simba.
Crescentius Magori aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba kabla ya nafasi yake haijachukuliwa na Senzo, amesema: “Utaratibu upo wazi, nilishangaa kuona mtendaji mkubwa kama yeye anashindwa kufuata weledi na kuibukia kwenye mitandao ya kijamii, lakini ukweli ni kwamba hawezi kuanza kufanya kazi huko alikokwenda mpaka watakapokuja mezani kuzungumza nasi.
“Kibali cha kazi kwa sasa kinaonyesha kuwa yeye ni mfanyakazi wa Simba, lazima tuthibitishe kwa kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani alikopewa kibali kisha tumruhusu aende huko anakotaka, hii haina ujanja ni utaratibu tu lazima Yanga waje tuwape kibali ili aanze kazi kwao.”