Na Saleh Ally
KILA mtu anaweza kuwa na kila anachokiamini tofauti na mwingine na hii ndiyo raha ya kupishana mawazo kwa kuwa kila mmoja anakuwa anaamini kile anachokiwaza na kukiamini.
Mimi naamini tofauti kabisa na wewe kwamba, fedha ambazo Yanga wanazitumia kwa ajili ya usajili zingeweza kutumika kuwapatia angalau uwanja wa mazoezi, basi lingekuwa jambo zuri sana.
Yanga wamefanya usajili wa zaidi ya Sh milioni 500, najua, itakuwa ni siri kwa kila kitu lakini uhalisia na wachezaji wanaowasajili, hakuna ubishi kwamba fedha zimetoka nyingi sana na kama kungekuwa na mpangilio mzuri yangefanyika yafuatayo na faida ingekuwa kubwa sana.
Nafuu:
Yanga imesajili wachezaji wa bei kubwa sana, mmoja hadi kafikia Sh milioni 220 na ni mchezaji mzalendo. Bado kulikuwa na nafasi kubwa ya Yanga kupata mchezaji wa aina hiyo kwa bei nafuu zaidi.
Unaona, beki kama Bakari Mwamnyeto akisajiliwa kwa zaidi ya Sh milioni 200, lakini Yanga inaweza kupata mchezaji kama huyo, mfano beki Ame, kasajiliwa kwa Sh milioni 35 na unaona tofauti ya kiwango na Mwamnyeto si kubwa sana.
Maana yangu ni hivi, wachezaji wanaosajiliwa wangeweza kuwa na ubora unaofanana na wale ambao wamesajiliwa kwa fedha kubwa ambayo ingebanwa kidogo na kiasi chake kupelekwa katika maandalizi ya uwanja.
Naendelea kusema ninaweza kuwa tofauti na wewe, najua ungetamani kuona ushindi wa uwanjani kwa kuwa haujui maumivu ya timu kujiandaa bila ya kuwa na uwanja wake wa mazoezi.
Yanga ina timu za vijana na wanawake, hizi zote haziwezi kuwa na maandalizi mazuri kama hakuna viwanja vya mazoezi. Hivyo naendelea kusisitiza hili jambo ni si sawa.
Mashabiki wanapenda ushindi lakini bado viongozi wanaweza kuwa na hesabu za kufikia mbali kwa kuwa kuwa na mchezaji mmoja wa zaidi ya Sh milioni 200, halafu usiwe na uwanja wa mazoezi pia ni matatizo.
Wataalamu wa usajili:
Lazima kuwa na timu sahihi ya usajili, lazima kuwa na watu wanaojua usajili utafanyika kwa ajili ya leo, kesho na baadaye. Maana usajili kama utakuwa kwa ajili ya kuwafurahisha wanachama tu leo, basi hilo ni tatizo kubwa sana.
Kinachofanyika Yanga ni kushindana zaidi na Simba, hili ni jambo zuri kwa kuwa linaleta maendeleo. Na wadhamini wa Yanga, GSM hakika wanajitahidi sana na wanastahili pongezi lakini kutubaliane kwa kuwa hakukuwa na skauti ya muda mrefu kupitia wataalamu, basi unaona mambo yatakuwa mazuri sasa lakini baada ya miaka miwili ijayo, Yanga itaendelea kubaki ilipo.
Nasema itabaki ilipo kwa kuwa mchezaji huenda akaondoka, huenda asielewane na uongozi au huenda mkataba wake utaisha atakwenda kwingine lakini Yanga itabaki ileile isiyokuwa na uwanja wake wa mazoezi.
Yanga haiwezi kuwa kubwa bila hata uwanja wa mazoezi, inaweza kuwa kongwe na maarufu kwa kuwa haikidhi vigezo vya kuwa kubwa.
Lazima kujifunza, kwa viongozi wanaojua wanafanya nini, maendeleo hayawezi kuwa ya leo pekee. Lazima kujipanga kwa ajili ya leo lakini muelekeo wa kesho uwe na uhakika.
Wakati mwingine unaangalia, Yanga haishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na huenda nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ni kuendelea kujenga timu, hili ni jambo sahihi. Lakini kama Yanga inataka kufanya bora zaidi kwa muda mrefu zaidi, uwanja ambayo ni sheria namba moja katika mchezo wa soka kati ya zile 17 ni muhimu sana.
Ukianza kutaja sheria 17 za mchezo wa soka, unaanza na uwanja. Hii inaonyesha kiasi gani uwanja unakuwa muhimu katika hili jambo.
Yanga tayari wana eneo kubwa sana ambalo walipewa zawadi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Maana yake kwa sasa hawahitaji kununua kiwanja kwa ajili ya kutengeneza uwanja wa mazoezi, badala yake ni suala la kuanza kuotesha nyasi, kutengeneza magoli lakini angalau sehemu ndogo ya kubadilishia nguo na baada ya hapo zinaweza kuanza hesabu za uwanja wa nyasi bandia. Sasa hapa inashindikana vipi?
Hesabu zingekuwa nzuri kwenye timu ya skauti, maana yake Yanga bado ingeweza kusajili wachezaji wazuri, wa kiwango kama hiki walichosajili na baada ya hapo ikapata angalau uwanja wa mazoezi ambao ungeweza kuanza kutumika wakati wa maandalizi ya mzunguko wa pili. Mtafakari.