UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa upo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo Septemba 11 wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo wa leo ni wa mzunguko wa pili ambapo Azam inaendelea kubaki nyumbani huku Coastal Union yenye maskani yake Tanga ikiendelea kukipiga ugenini.
Mchezo wa kwanza, Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba ilishinda kwa bao 1-0 mbele ya Polisi Tanzania na ilikuwa ni Uwanja wa Azam Complex.
Coastal Union inaingia uwanjani ikiwa imetoka kuchapwa bao 1-0 mbele ya Namungo FC kwenye mchezo uliochezwa, Lindi Uwanja wa Majaliwa.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa kila kitu kipo sawa na wanahitaji pointi tatu mbele ya Coastal Union.
“Ni mchezo mgumu ila tupo tayari kwa ajili ya mechi yetu dhidi ya Coastal Union, wachezaji wapo vizuri wanahitaji kuendelea kutoa burudani, mashabiki wajitokeze kutoa sapoti,” amesema.
Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Coastal Union amesema kuwa licha ya kupoteza mchezo wa kwanza bado wana nguvu ya kuendelea kupambana.