UONGOZI wa Yanga umesema kuwa upo tayari kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Mbeya City unaotarajiwa kuchezwa Septemba 13, Uwanja wa Mkapa.
Yanga itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya Tanzania Prisons mchezo uliochezwa Septemba 6, Uwanja wa Mkapa.
Mbeya City wao wataingia uwanjani wakiwa wametoka kupoteza kwa kufungwa mabao 4-0 mbele ya KMC, Uwanja wa Uhuru.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mechi zao zote zilizo mbele yao hivyo watapambana kupata pointi tatu.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa msimu uliopita wa 2019/20 timu zote mbili zilitoshana nguvu kwenye mechi zao zote mbili walizokutana ndani ya uwanja.
Ule wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya ngoma ilikamilika kwa sare ya bila kufungana na ule wa pili uliochezwa Uwanja wa Mkapa ulikamilika kwa kufungana bao 1-1.