ZIMEBAKI takribani siku 28 kwa sasa kufika Oktoba 18 tushuhudie miamba ya soka Bongo, Yanga na Simba ikipambana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Ikiwa kwa sasa tupo mzunguko wa tatu ndani ya Ligi Kuu Bara, rekodi zinaonesha kuwa kwa mzunguko wa kwanza na wa pili, nyota wa Yanga, Michael Sarpong amewafunika mastaa wote wa Simba.
Sarpong amekuwa na moto, ambapo ndani ya dakika 180 ambazo ni mechi mbili, ameingia ndani ya 18 mara 34 akipiga jumla ya pasi 70, akichezewa faulo mara tatu, huku yeye akicheza faulo mbili.
Sarpong mbele ya Mbeya City, alipiga pasi 40, aliwatoka mabeki mara 9, alicheza faulo 2, akachezewa faulo 1. Alisababisha kona 1, aliingia ndani ya 18 mara 23 na aliotea mara moja.Dhidi ya Prisons, alipiga pasi 30, ndani ya 18 aliingia mara 11, alichezewa faulo 2 na alifunga bao moja.
Mechi zote zilikuwa Uwanja wa Mkapa.Kwa upande wa Simba, wanaye Bernard Morrison ambaye amecheza kwa dakika 133. Yeye ameingia ndani ya 18 mara 29, amepiga kona 3, amechezewa faulo mara 5.
Matukio hayo yalikuwa Uwanja wa Sokoine, wakati Simba ikishinda mabao 2-1, alisababisha kona 1, alipiga kona 3, aliingia ndani ya 18 mara 10, alicheza faulo 1.
Mbele ya Mtibwa Sugar, wakati Simba ikibanwa mbavu kwa kufungana bao 1-1, Morrison aliingia ndani ya 18 mara 19, alichezewa faulo 5, aliwatoka mabeki mara 3, alicheza faulo 1, akapiga faulo moja.
Nyota mwingine ambaye anapewa nafasi ya kufanya makubwa ni kiungo raia wa Angola, Carlos Carlinhos ambaye kabla ya jana, alicheza mechi moja dhidi ya Mbeya City pale Uwanja wa Mkapa.Katika mchezo huo, alipiga jumla ya pasi 15, kona 5 na ana akatoa asisti moja kwa Lamine Moro.
Yanga ikishinda 1-0.Luis Miqussone wa Simba, amecheza mechi moja kati ya mbili ambazo timu yake imecheza. Ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar, alipiga kona 4, akachezewa faulo 3.
Tuisila Kisinda ndani ya dakika 180 kabla ya jana, alipiga jumla ya pasi 60. Mbele ya Prisons zilikuwa pasi 23, alisababisha kona 1, akawatoka mabeki mara 1.Mbele ya Mbeya City, alipiga pasi 37, aliwatoka mabeki mara 6, alichezea faulo 1.
Huyu vita yake ni dhidi ya Clatous Chama ambaye mbele ya Mtibwa Sugar, alimsababishia kadi ya njano kiungo Baraka Majogoro na ana pasi moja ya bao iliyopatikana kwa Ihefu wakati Simba ikishinda mabao 2-1.