MTENDAJI Mkuu wa Klabu ya Gwambina ya Misungwi mkoani Mwanza, Mwinyi Zahera amesema katika mechi yao dhidi Simba chochote kinaweza kikatokea kwa kuwa Simba ni timu kubwa nchini lakini kikosi chake kipo tayari kukabiliana nao leo Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Zahera amesema pamoja na ubora wa kikosi cha Simba pamoja na kuwa na wachezaji wenye viwango vikubwa nchini, kamwe hawezi kutishika na ukubwa huo: “Mimi nimeshacheza na Sadio Mane, Mohamed Salah lakini sikuwaogopa vipi nije kuwaogopa kina Kagere na Chama ingawa ni wachezaji wazuri?
Nawaheshimu lakini siwezi kuwaogopa,” amesema Zahera.
Aidha, kocha huyo amesema ili waone ukubwa wa Simba basi wawafunge zaidi ya goli nane kwa kuwa hata Barcelona waliwahi kufungwa goli nane na Buyern Munich ya Ujerumani katika nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya mwezi Agosti 2020.
Itakumbukwa Kocha Mwinyi Zahera aliwahi kuifundisha klabu kongwe nchini Yanga msimu wa 2018-19 na katika msimu wa 2019-20 alifungashiwa virago kutokana na kuwa na mwendelezo mbovu wa matokeo katika msimu wake wa mwisho.
Gwambina bado haijapata ushindi katika michezo mitatu iliyopita ambayo walipata suluhu dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kufungwa na Ruvu Shooting na Biashara ya Mara huku ikiwa haijafunga goli hata moja.