MLINDA mlango namba moja ndani ya Klabu ya Simba, Aishi Manula amenyooshwa mazima ndani ya dakika 360 alizokaa langoni na kipa namba moja wa Azam FC, David Kissu kwa kupotezwa kulinda lango lake bila kuruhusu bao,’Clean Sheet’.
Manula anakibarua cha kutetea tuzo yake ya kipa bora ambayo aliipata msimu uliopita wa 2019/20 baada ya kuanza kwa kuyeyusha ‘cleansheet’ za mwanzoni kabisa.
Mechi mbili mfululizo ugenini mbele ya Ihefu wakati Simba ikishinda 2-1 Uwanja wa Sokoine na ule Uwanja wa Jamhuri wakati Simba ikilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 alitunguliwa na amejikusanyia ‘cleansheet’ mbili Uwanja wa Mkapa ilikuwa mbele ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 4-0 na mbele ya Gwambina wakati Simba ikishinda mabao 3-0.
Kwa upande wa Kissu wa Azam FC amempoteza mazima Manula kwa kuwa mechi zake zote nne alizokaa langoni nyavu zake hazijatikishwa ndani ya dakika 360.
Alianza mbele ya Polisi Tanzania wakati Azam ikishinda ba 1-0, mbele ya Coastal Union wakati Azam ikishinda mabao 2-0 Uwanja wa Azam Complex na walipotoka mkoani alianza mbele ya Mbeya City wakati Azam FC ikishinda bao 1-0 Uwanja wa Sokoine na mbele ya Tanzania Prisons wakati Azam FC ikishinda bao 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela.
Aanayemfuatia kwa ukaribu ni Metacha Mnata wa Yanga ambaye amekaa langoni kwenye mechi tatu na zote ameweka lango lake salama.
Ilikuwa ni mbele ya Mbeya City wakati Yanga ikishinda bao 1-0, Kagera Sugar 0-1 Yanga na Mtibwa Sugar 0-1 Yanga.