MCHEZO uliopangwa kuchezwa Oktoba 9 kati ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, Azam FC dhidi ya Mwadui FC umesogezwa mbele mpaka Oktoba 15.
Ofisa Habari wa Azam FC Zakaria Thabit, amesema kuwa wamepokea taarifa hizo za kusogezwa mbele mechi hizo ila walikuwa na uwezo wa kucheza bila tatizo.
Thabit amesema:-“Ndugu zangu, mechi yetu na Mwadui FC iliyopaswa kuchezwa Oktoba 9 imesogezwa mbele mpaka Oktoba 15.
“Lakini hata hivyo, hata kama isingesogezwa, tungecheza tu. Kumbuka sisi ni Azam FC, siyo Simba wala Yanga.”
Mchezo wa Yanga na Simba ambao ulikuwa unatarajiwa kuchezwa Oktoba 18, umepelekwa mbele mpaka Novemba 7, leo Oktoba 7 na Bodi ya Ligi Tanzania. Azam FC ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 15 na imecheza mechi 5, haijapoteza mchezo mpaka sasa.
Mwadui ikiwa imetoka kushinda bao 1-0 dhidi ya Namungo FC itakutana na Azam FC iliyotoka kushinda mabao 4-2 dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Azam Complex.