SAHAU kuhusu umri wake wa miaka 33, imebainika kwamba thamani ya jembe jipya la Yanga, Saidi Ntibazonkiza raia wa Burundi ni kufuru kwani amewafunika nyota wote wa Bongo wakiwemo viungo wa Simba, Luis Miquissone na Clatous Chama.
Kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market, ambao unajihusisha na masuala mbalimbali ya wachezaji ikiwemo thamani zao, Ntibazonkiza ana thamani ya Euro 550,000 ambazo ni sawa na Sh bilioni 1.5, ikiwa hakuna nyota mwingine Bongo anayefikia kiasi hicho.
Nyota huyo wa zamani wa Vital’O ya Burundi, alitambulishwa Oktoba 12 na Yanga ikiwa ni usajili wao mpya baada ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.
Thamani ya Ntibazonkiza aliyefunga bao pekee la Burundi wakati ikicheza na Taifa Stars kwenye mechi ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Oktoba 11 inazidi ile ambayo ilitumiwa na Simba kusajili timu nzima msimu wa 2017/18, ambapo wenyewe waligota Sh bilioni 1.3.
Ukiwajumisha nyota kama Aishi Manula, John Bocco, Erasto Nyoni na wengineo.
Wakati Ntibazonkiza akiwa na thamani hiyo Chama thamani yake ni Euro 100,000 (Sh 273,170,000) na Miquissone ni Euro 150,000 (Sh 409,755,000) kuonyesha kuwa jamaa huyo wa Burundi kawatupa mbali na kwenye timu za Bongo hakuna mchezaji ambaye mtandao huo unaonyesha kuwa anamfikia.