LAMINE Moro nahodha wa Yanga amesema kuwa kikosi kipo tayari kwa ajili ya mechi zao za Ligi Kuu Bara kwa kuwa wamempata mwalimu mpya ambaye yupo vizuri hivyo jukumu la mashabiki ni kuwapa sapoti katika mechi zao.
Yanga leo inacheza mchezo wa ligi dhidi ya KMC utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba saa 10:00 jioni.
Mchezo wa leo utakuwa ni wa saba kwa Yanga huku ukiwa ni mchezo wa pili kwa Kocha Mkuu, Cedric Kaze ambaye mchezo wake wa kwanza ilikuwa dhidi ya Polisi Tanzania na alishinda bao 1-0.
Lamine amesema:”Kila kitu kipo sawa na kikubwa tunachoomba ni sapoti kutoka kwa mashabiki katika mechi zetu zote ambazo tutacheza kwani ushindani ni mkubwa.
“Kila mchezaji anajua kwamba kwa sasa tupo na mwalimu mpya hivyo licha ya kwamba bado hajawa na mechi nyingi ana kitu cha kutupa nasi pia tuna kazi ya kuwapa ushindi mashabiki.”
Lamine ni kinara wa utupiaji ndani ya Yanga kwa upande wa mabeki akiwa nayo mabao mawili na Yanga ikiwa imefunga jumla ya mabao nane kibindoni
Ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 16 na kinara ni Azam FC mwenye pointi 21 baada ya kucheza mechi 7 ndani ya Ligi Kuu Bara huku mabingwa watetezi Simba wakiwa nafasi ya tatu na pointi 13 baada ya kucheza mechi sita.