UONGOZI wa Mtibwa Sugar umesema kuwa kikubwa ambacho kinawabeba ndani ya uwanja ni juhudi na kujituma kwa wachezaji wao matokeo mabaya ilikuwa ni mpito kwao.
Imekuwa ya kwanza kuitungua Klabu ya Azam FC kwa msimu wa 2020/21 ambayo ilicheza mechi saba bila kupoteza ambapo umeweka bayana kuwa wapinzani wao walikuwa wanakutana na timu ndongo ndio maana walikuwa wanashinda.
Mtibwa Sugar inayonolewa na Kocha Msaidizi, Vincent Barnaba imekuwa kwenye mwendo wa tofauti kwa msimu wa 2020/21 baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Zuber Katwila kubwaga manyanga na kuibukia ndani ya Ihefu FC.
Barnaba amekiongoza kikosi hicho kwenye mechi mbili ambapo alisepa na pointi sita Uwanja wa Jamhuri, Morogoro ilikuwa ni mbele ya Namungo FC ambapo timu ilishinda bao 1-0 na mbele ya Azam FC ilishinda bao 1-0.
Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema kuwa Mtibwa Sugar ni chuo cha mpira na kila mchezaji anayecheza hapo anajua namna ya kufanya.
“Unajua sisi Mtibwa Sugar ni chuo cha mpira na vijana wetu wanaingia darasani kujifunza, tupo imara muda wote huwa hatubahatishi katika kazi yetu.
‘Kuifunga Azam hilo tuliweka wazi mapema, tunajua kwamba walikuwa hawajafungwa ila walikuwa wanakutana na timu ndogondogo, sasa wamekutana na timu kubwa tumefanya yetu na kuchukua pointi tatu.
“Matokeo mabovu ambayo tulikuwa tunayapata nyuma yalikuwa yanatukasirisha kwani yalikuwa yanatokea bila sababu,ukianzia kwa wachezaji wanalipwa vizuri na kwa wakati, kambi safi na kila kitu kipo hivyo kwa sasa tumeanza kurejea kwenye ile kasi yetu,” amesema.
Mtibwa Sugar imecheza jumla ya mechi 8, imeshinda mechi 3 imepoteza mechi tatu na kuambulia sare mbili ikiwa nafasi ya 10 na pointi 11.