TARATIBU mbinu za wazungu zinaanza kufeli mbele ya wazawa ambao wanazinoa timu zao kwa kubeba pointi tatu mbele ya makocha wakigeni.
Oktoba 22, Tanzania Prisons inayonolewa na mzawa Salum Mayanga alikiongoza kikosi chake kuitungua Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji.
Kwenye mchezo huo Prisons ilishinda bao 1-0 dhidi ya Simba Uwanja wa Nelson Mandela, Oktoba 26, Simba ilinyooshwa tena na Ruvu Shooting inayonolewa na Charles Mkwasa ambaye ni mzawa kwa ushindi wa bao 1-0.
Ndani ya dakika 180 mbinu za Sven zimekwama kwa wazawa wawili ambapo amefungwa mabao mawili huku safu yake ya ushambuliaji ikishindwa kufunga.
Kwa upande wa vinara wa Ligi Kuu Bara, Azam FC iliyo chini ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba ilipoteza mchezo wake wa kwanza kwa kufungwa bao 1-0 Oktoba 26, Uwanja wa Jamhuri Morogoro na Vincent Barnaba kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar ambaye ni mzawa.
Azam FC ilikuwa imecheza mechi saba ambazo ni dakika 630 bila kupoteza na ilifungwa mbele ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa nane na kuyeyusha pointi tatu kwa mara ya kwanza kwa msimu wa 2020/21.