BAADA ya kupachika bao lake la kwanza akiwa ndani ya Yanga, Wazir Junior amesema kuwa hesabu zake ni kuona timu hiyo inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/21.
Junior ambaye alijiunga na Yanga kwa dili la miaka miwili akitokea Klabu ya Mbao alipachika bao hilo kwenye mchezo dhidi ya KMC wakati Yanga ikishinda mabao 2-1.
Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba ulikuwa ni kwanza kwake kuanza kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mkuu Cedric Kaze.
KMC ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Hassan Kabunda liliwekwa sawa na Tuisila Kisinda kwa mkwaju wa penalti kisha Junior alipachika bao la ushindi lililoipa Yanga pointi tatu mazima.
Anakuwa mzawa wa kwanza kufunga ndani ya Yanga ambayo imefunga mabao 10 baada ya kucheza mechi saba.
“Ni furaha kwangu kufunga na nilikuwa ninafikiria jambo hili kwa muda mrefu, kwa kuwa nimefunga bao langu la kwanza basi ninafikiria kuona timu inatwaa ubingwa wa ligi kwa msimu wa 2020/21.
“Kila kitu kinawezekana kwa kuwa wachezaji tunajituma na kila anayepata nafasi anaonyesha uwezo wake kwa kufanya kazi kwa juhudi,” amesema.
Yanga ipo nafasi ya pili kwenye ligi ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi saba kwa msimu wa 2020/21.