ARSENAL ipo kwenye mpango wa kuongeza mkataba kiungo Mohamed Elney kwa ajili ya kuendelea kukitumikia kikosi hicho kwa msimu ujao.
Kiungo huyo raia wa Misri ameonekana kuwa bora ndani ya Arsenal, jambo ambalo limemfanya Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta kuhitaji kupata huduma yake kwa msimu ujao na yupo kwenye mpango ndani ya kikosi hicho.
Elney mwenye miaka 28 alikuwa kwenye kikosi kilichoshinda bao 1-0 dhidi ya Manchester United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Old Trafford na aliweka bayana kuwa walitambua kwamba wangeshinda mchezo huo kabla ya kipindi cha kwanza.
Arteta amesema amempa chaguo la kwanza kiungo huyo aliyekuwa anacheza kwa mkopo ndani ya Klabu ya Besiktas na anaamini itakuwa vema ikiwa atakubali kuongeza mkataba ndani ya kikosi hicho.
“Nipo na furaha kwa ajili yake na nina amini kuwa anaweza kuwa sehemu ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao kwa hapa ambapo tumefikia, ni kiungo makini na atakuwa msaada kwenye timu,” amesema.