KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema kuwa walistahili kupewa penalti kwenye Dar Dabi iliyochezwa Novemba 7 Uwanja wa Mkapa na timu zote kuambulia pointi mojamoja baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
Yanga ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo walianza kupata bao la kuongoza dakika ya 31 kupitia kwa Michael Sarpong kwa mkwaju wa penalti uliompoteza mlinda mlango namba moja wa Simba Aishi Manula na lile la Simba lilifungwa na Joash Onyango.
Onyango ambaye ni beki kisiki ndani ya Simba alifunga bao hilo dakika ya 86 na kumfanya afute makosa aliyoyafanya dakika ya 28 na kufanya Yanga wapewe penalti kwa kuwa mwamuzi wa kati Abdalah Mwinyimkuu alitafsri kwamba alimchezea faulo Tuisila Kisinda.
Sven amesema kuwa:”Kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga nafikiri tulipaswa kupewa penalti kwa kuwa wachezaji wangu walichezewa madhambi mengi na wapinzani wetu.
“Lakini kwa kuwa ni mpira na maamuzi yameshatolewa basi ni wakati wetu wa kufanya maandalizi kwa ajili ya wakati ujao ili kuzidi kuwa bora.
“Ligi ina ushindani na kila mmoja anahitaji ushindi hivyo mashabiki wazidi kutupa sapoti kwani kazi ipo na tutazidi kupambana ili kuwa bora,” amesema.
Simba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza mechi 10 ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21.
Vinara ni Azam FC wenye pointi 25 huku nafasi ya pili ipo mikononi mwa Yanga yenye pointi 24 zote zimecheza mechi 10.