BONDIA Hassan Mwakinyo na Muargentina Jose Carlos Paz wametamba kila mmoja atamchapa mwenzake katika pambano la kuwania ubingwa wa uzito wa Super-Welter wa mabara unaotambuliwa na chama cha WBF.
Mwakinyo na Paz watapambana Ijumaa kwenye ukumbi wa Next Door Arena katika pambano lililopangwa kuwa la raundi 12.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari Mwakinyo amesema kuwa atahakikisha Paz anaachana na mchezo wa ngumi za kulipwa kutokanana kipigo alichumuandalia.
“Natamani pambano lifanyike mapema iwezekanavyo, hata siku moja kabla kwani nipo fiti zaidi ya nilivyokuwa mwanzoni. Sitaki kuwanyong’onyesha Watanzania katika pambano hilo,” amesema Mwakinyo.
Amesema kuwa anajua kuwa Paz ni bondia mzuri na amejiandaa vyema katika pambano hilo, lakini kutokana na jinsi alivyojiandaa, hatakuwa na nafasi ya kutamba kwake.
Kwa upande wake, Paz amesema kuwa hakuja nchini kutembea zaidi ya kuwania ubingwa ambao Mwakinyo anao.
“Nipo vizuri, mazoezi yangu nchini yamekuwa na mafanikio makubwa na hali ya hewa siyo tatizo. Nitamfundisha ngumi Mwakinyo ,” amesema Paz.
Kwa mabondia hao kutambiana pia bondia Hussein Itaba na mpinzani wake kutoka DR Congo, Alex Kabangu, Fatuma Zarika dhidi ya Patience Mastara (Zimbabwe) na Mtanzania Zulfa Macho ambaye atazichapa na Alice Mbewe wa Zambia pia walitambiana.
Mkurugenzi wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema kuwa maandalizi yamekamilika na kuwaomba mashabiki kuendelea kununua tiketi kwa ajili ya pambano hilo.
“Maandalizi yapo vizuri na kama mnavyoona mabondia wote wapo hapa na sas tunamsubiri Rais wa WBF, Howard Goldberg na mwamuzi Edward John Marshall ambao watawasili kesho Jumatano Novemba 11,” amesema Twisa.
Twissa amesema tiketi zitaanza kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa Sh 3 Milioni kwa meza ya watu 10 na Sh150,000 kwa kwa viti vya kawaida.