UONGOZI wa Simba umeweka bayana kwamba utawashangaza wengi kwenye kazi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa wanaiwakilisha nchi kwenye mashindano makubwa jambo ambalo wanaamini litatimia.
Simba imepata nafasi ya kuwa wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2019/20 wakiwa na pointi 88 baada ya kucheza mechi 38.
Inakutana na vigogo kutoka Nigeria, Plateu United ambao wapo vizuri kwenye safu ya ushambuliaji kwa kuwa msimu huu kwenye mechi zake tatu imefunga jumla ya mabao 14, waliifunga Enyimba 0-4,5-0 Adamawa United na 5-1 Ifeanyi Uba hivyo wawakilishi wanakazi ya kufanya.
Mchezo wa kwanza kwa Simba unatarajiwa kuchezwa kati ya Novemba 27-29 Uwanja wa New Jos nchini Nigeria na ule wa pili unatarajiwa kuchezwa kati ya Desemba 4-6 Uwanja wa Mkapa.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa kikubwa ambacho wanakihitaji kwa sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni kufika mbali.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya na Ligi ya Mabingwa Afrika sio kitu chepesi ni lazima tufanye kazi kubwa kufikia pale ambapo tunahitaji, kikubwa ambacho tunakitaka ni kuweka rekodi nzuri tofauti na msimu uliopita,” amesema.
Msimu uliopita, Simba iliishia hatua za awali baada ya kutoshana nguvu na Klabu ya UD Songo kwenye mechi zote mbili ambapo ile ya mwanzo ugenini zilitoshana nguvu ya bila kufungana na Uwanja wa Mkapa walifungana bao 1-1.