ETIENNE Ndayiragije, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa kutokana na maandalizi ambayo wameyafanya wana imani ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa kufuzu Afcon kesho, Novemba 13.
Stars iliweka kambi ya muda wa siku tatu nchini Uturuki ikiwa ni maandalizi ya mchezo huo wa kesho ambao utachezwa bila ya uwepo wa mashabiki kutokana na Shirikisho la Soka Afrika,(Caf) kutaka iwe hivyo ili kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona.
Utachezwa Uwanja wa Olympique de Rades nchini Tunisia na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa Novemba 17, Uwanja wa Mkapa na umeruhisiwa kuwa na nusu ya mashabiki na Caf wenyewe.
Ndayiragije kwenye mchezo wa kesho atawakosa washambuliaji wawili ambao ni pamoja na Adam Adam yeye ni mzawa alikosa paspoti ya kusafiria pamoja na Mbwana Samatta ambaye anasumbuliwa na maumivu ya msuli.
Kocha huyo amesema:”Kila kitu kipo sawa kwa maandalizi ambayo tumeyafanya nina amini kwamba tutapata matokeo chanya licha ya kwamba tutakuwa ugenini.
“Kikubwa tunatambua kwamba hatutakuwa na Samatta ila wapo wachezaji wengine ambao watacheza kwa niaba yake na nina amini kwamba watapambana ili kufanya vizuri kwani matokeo yakiwa mazuri ni furaha kwa kila mmoja,” .
Stars ipo kundi J ina pointi tatu ikiwa inakutana na Tunisia ambao ni vinara wakiwa na pointi sita hivyo ikishinda itaongeza nafasi ya kunusa hatua ya kufuzu Afcon 2021 nchini Cameroon.
Tayari kikosi kimeshawasili nchini Tunisia ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa kesho.