KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck pamoja na mabosi wa timu hiyo kwa sasa wanaweza kuanza kufurahia kupangiwa na Plateau United FC ya Nigeria kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na sababu tano ambazo zinawapa nafasi ya kusonga mbele.
Hata hivyo, mashabiki wa Yanga hawatakuwa na nafasi ya kuwazomea Simba kwa kuwa mechi zote hazitakuwa na mashabiki kutokana na janga la Corona. Simba wamepangwa kuanza na Plateau United kwenye hatua ya awali ya michuano hiyo mikubwa Afrika ambapo wataanzia ugenini nchini Nigeria Novemba 27- 29 kabla ya kurudiana Desemba 4-9 jijini Dar.
Wakati kikosi hicho cha Simba kikianza maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo hizi hapa ni sababu tano ambazo zinawapa nafasi ya kusonge mbele dhidi ya wapinzani wao;- Kutocheza kwa muda mrefu
Hii ni sababu kubwa sana ambayo inawapa matumaini Simba ya kuwachapa wapinzani wao kwenye mechi hizi mbili.
Plateau hawajacheza mechi yoyote ya kiushindani tangu mwezi Machi baada ya ligi hiyo kusimamishwa kutokana na Virusi vya Corona. Wakati Plateau United wakiwa hawana ufiti wa kucheza mechi Simba wao wamecheza mechi za Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na zile za kirafiki ambazo zinawapa muda wachezaji kuzoeana na kocha kutambulisha mifumo na mbinu anazozitumia vizuri kwa sasa wakiwa wameshacheza michezo 10 ya ligi.
Uchanga wao kwa Simba
Plateau United licha ya kuwa ni timu imara na bora kwa Nigeria lakini siyo timu kubwa nchini humo kulinganisha na Enyimba. Lakini pia wameachwa mbali kiukongwe na Simba hasa katika kushiriki michuano hiyo mara kwa mara.
Mara ya mwisho walishiriki michuano hii ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2018, wakati Simba ilikuwa msimu uliopita. Simba ilianzishwa mwaka 1936 wakati Plateau United ikianzishwa 1975.
Corona imewapa nafasi
Plateau United walipata zali ya kutangazwa kuwa mabingwa wa Nigeria kutokana na mlipuko wa Virusi vya Corona baada ya kuwa kileleni mwa msimamo wakiwa mbele ya Enyimba. Kama ligi ingeendelea na Corona ingeisha yawezekana wasingepata mafanikio ambayo wanayo kwa sasa kwa kuwa ligi yao ilifutwa.
Mechi hazina mashabiki
Uzuri wa mechi zote mbili hazitakuwa na mashabiki jambo ambalo linaweza kuwa faida zaidi kwa Simba kutokana na kuwaepuka mashabiki wa wapinzani wao kule Nigeria na hapa nchini hasa wale wa Yanga.
Chama, Kagere kuwabeba
Jambo la tano ambalo linawapa uhakika Simba wa kusonga mbele dhidi ya wapinzani wao ni kuwa na mchanganyiko wa wachezaji wengi wa kigeni wenye uzoefu na michuano hii.
Simba ina mchanganyiko wa wachezaji wa kigeni wakiwemo Meddie Kagere na Clatous Chama wakati Plateau United wana mchezaji mmoja pekee ambaye anatoka nje ya taifa hilo.
Licha ya mambo hayo matano kuipa Simba nafasi, timu hii siyo ya kubeza maandalizi yanahitajika.