PRINCE Dube, raia wa Zimbabwe leo amefunga bao la kusawazisha kwa timu yake ya Taifa wakati ikilazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Algeria kwenye mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu Afcon uliochezwa leo Novemba 16, Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe.
Dube anayecheza ndani ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara alifunga bao hilo lililoipa pointi moja timu yake dakika ya 82 zikiwa zimebaki dakika nane mpira kukamilika.
Algeria ilikuwa ya kwanza kufunga dakika ya 34 kupitia kwa Andy Delort na lile la pili lilifungwa na Riyad Mahrez dakika ya 38. Bao la kwanza kwa Zimbabwe lilifungwa na Knowledge Musona dk ya 43 na ubao ukawekwa sawa na Dube dk ya 82.
Dube mpira wake wa kwanza kuugusa ulizama kambani kwa kuwa alitoka kuingia dakika ya 81 akichukua nafasi ya Darikwa.
Matokeo hayo yanaifanya Zimbabwe kufikisha jumla ya pointi 5 ikiwa nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikiwa chini ya Algeria wenye pointi 10 na Zambia anayocheza Clatous Chama ikiwa nafasi ya nne na pointi tatu na nafasi ya tatu ipo mikononi mwa Botswana yenye pointi nne zote zimecheza mechi nne.