BAADA ya Hitimana Thiery, aliyekuwa kocha mkuu wa Namungo kufutwa kazi Novemba Novemba 18 na mikoba yake kuchukua Hemed Morocco ameweka wazi kuwa hakukuwa na maelewano kati yake na mabosi wa timu hiyo.
Thiery alikiongoza kikosi hicho kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2018/19 na msimu wake wa kwanza ndani ya ligi aliweza kukiongoza kikosi hicho kumaliza ligi kikiwa nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 38 na kilikusanya pointi 64.
Kwa msimu wa 2020/21 amekiongoza kikosi hicho kucheza mechi 10 na kukusanya pointi 14 kikiwa nafasi ya tisa na aliweka wazi sababu ya kuboronga kwake ni kukosa muda wa maandalizi pamoja na wachezaji wake wengi tegemezi kusumbuliwa na majeraha.
Akizungumza na Salleh Jembe, Thiery ambaye alikifikisha kikosi cha Namungo hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Simba amesema kuwa ikiwa watu wawili wakiachana ina maana hawaelewani.
“Ikiwa watu wawili wameachana ina maana kuna jambo hawaelewani, sitaki kuzidisha hapo juu ya hilo niliiishi Namungo, Namungo vizuri kabisa huenda ni muda, sina cha kusema zaidi ya asante,” amesema Thiery.
Licha ya Namungo kupoteza kwa kufungwa na Simba fainali ya Kombe ka Shirikisho Uwanja wa Nelson Mandela itaiwakilisha nchi kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho kwa kuwa Simba wataiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na itacheza na Al Rabita ya Sudan Kusini Novemba 28, Uwanja wa Azam Complex.
Leo Namungo ikiwa chini ya Hemed Morocco kwa mara ya kwanza atakiongoza kikosi hicho kusaka pointi tatu mbele ya Yanga.