WAENDESHA mashitaka nchini Argentina wanamchunguza daktari wa Diego Maradona, Leopoldo Luque, wakimshuku kwa kuua kufuatia kifo cha nyota huyo wa soka kilichotokea Novemba 25 mwaka huu.
Polisi mjini Buenos Aires wameisaka nyumba na kliniki ya daktari huyo huku wakijaribu kubaini iwapo ulikuwepo uzembe katika matibabu baada ya upasuaji aliofanyiwa Maradona.
Maradona ambaye alikuwa na umri wa miaka 60 alifariki dunia kutoka na shinikizo la damu nyumbani kwake ambako alikuwa akiendelea kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.
Polisi wanashuku kwamba nyota huyo wa soka aliruhusiwa kwenda nyumbani kwake akiwa bado hajatimiza masharti ya kumruhusu atoke hospitalini, ikiwemo kupewa wauguzi au nesi wa kumhudumia saa 24, wataalamu wa uraibu, kupewa daktari anayeweza kumuita wakati wowote na gari la kubebea wagonjwa lenye vifaa vya kumsaidia kupumua.
Maafisa wanataka kufahamu kuhusu uhusika wa daktari Luque katika mipango ya kupona kwa Maradona katika nyumba ya nyota huyo.
Maradona alifanyiwa upasuaji kwenye mshipa wa ubongo kutokana na kuganda kwa damu ambapo mapema mwezi wa Novemba alikuwa akipata matibabu kutokana na uraibu wa pombe.
Familia ya Maradona inafuatilia kwa makini sakata hilo ili kubaini kama dakatari huyo alifanya uzembe wakati wa upasuaji.