JUMA Mgunda, Kocha Mkuu wa Coastal Union amesema kuwa kutokana na safu yao ya ulinzi kufanya makosa yanayojirudia atatumia dirisha dogo kusajili mabeki wazuri pamoja na washambuliaji.
Coastal Union ikiwa imecheza mechi 13 imefungwa jumla ya mabao 18 na safu ya ushambuliaji imefunga mabao 9 kwa msimu wa 2020/21.
Inashikilia rekodi ya kuwa timu iliyofungwa mabao mengi ndani ya uwanja kwa msimu huu ambapo ilifungwa mabao 7-0 dhidi ya Simba.
Mgunda amesema kuwa makosa ambayo wamekuwa wakiyafanya ndani ya uwanja yamewafanya washindwe kupata matokeo chanya jambo ambalo litawalazimu kufanya usajili.
“Kweli mambo sio mazuri, tumekuwa tukifanya makosa ya mara kwa mara, ninaweza kusema kwamba kuondoka kwa nyota wetu Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Ame kwa kiasi fulani yameturudisha nyuma ila maisha lazima yaendelee.
“Kuelekea kwenye dirisha dogo nina amini kwamba tutaboresha kikosi chetu kuanzia kwa ushambuliaji pamoja na ulinzi ili kuweza kuwa imara ndani ya ligi,” amesema.
Coastal Union ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 16 ndani ya Ligi Kuu Bara na kinara ni Yanga mwenye pointi 31 baada ya kucheza mechi 13.
Dirisha dogo ndani ya Bongo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15.