NORMAN Mapeza, Kocha Mkuu wa FC Platinum ya Zimbabwe, amesema kuwa anatambua uimara wa Simba upo kwenye safu ya kiungo na ushambuliaji, jambo ambalo atalifanya ni kuongeza nguvu kwenye ulinzi na safu yake ya ushambuliaji.
Safu ya ushambuliaji ya Simba inaongozwa na John Bocco mwenye mabao nane huku wapishi wa mabao hayo wakiwa ni viungo Luis Miquissone, mwenye pasi saba (asisti) na bao moja pamoja na Clatous Chama mwenye asisti nane na mabao sita ndani ya Ligi Kuu Bara.
Mapeza alikiongoza kikosi chake kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Taifa Zimbabwe kushinda bao 1-0, ana kibarua cha kulinda ushindi huo ili atinge hatua ya makundi huku Simba wakiweka wazi kwamba lazima wapindue meza kibabe kesho Jumatano, Uwanja wa Taifa, Dar.
Mchezo huo wa kesho Januari 6 utachezwa majira ya saa 11:00 jioni.
Mapeza amesema kuwa anatambua uimara wa Simba ulipo kwa kuwa aliwaona walipocheza kwenye mchezo wao wa kwanza, hivyo presha yake ni kwenye viungo.
“Ninawatambua wapinzani wangu, niliwaona kwenye mchezo wetu uliopita na nguvu yao kubwa ipo kwenye viungo hapo ndipo uimara wao ulipo pamoja na safu ya ushambuliaji ambayo ina nguvu.
“Kwangu mimi naona ni sawa hata nikiwa ugenini nina nafasi ya kupata matokeo, timu kubwa duniani zikiwa ugenini zinashinda na zikiwa nyumbani pia zinapoteza, nimewaambia vijana wangu namna ya kuwazuia na tutashambulia bila kuogopa,” amesema.
Chanzo: CHAMPIONI