HATIMAYE ni wakati mwingine tena kwa ajili ya kuendelea na mapambano ndani na nje ya uwanja kwa wawakilishi wetu kusaka tiketi ya kusonga mbele kwenye michuano ya kimataifa.
2020 ilikuwa na maumivu kwa timu zetu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kutokana na kupata matokeo ambayo hayakuwa na furaha kwao pamoja na mashabiki.
Ukianza na Namungo FC ambao mchezo wa kwanza walikuwa nyumbani licha ya kushinda mabao 2-0 bado furaha haikuwepo kwenye sura zao.
Ukweli ni kwamba ushindi wa mabao hayo nyumbani ni mwanzo tu kwa sababu mechi bado haijaisha hasa baada ya kumaliza dakika 90 za mwanzo.
Kazi kubwa inaanza upya kwa kuwa ni wakati wa kwenda kusaka ushindi na safari hii Namungo inayowakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho itakuwa ugenini.
Soka letu la Afrika lipo wazi kwamba kila mtu ashinde mechi zake hasa za nyumbani. Kasumba ya kwamba nafasi ya kushinda ugenini ni kubwa hiyo kwetu ni finyu na ni asili yetu tuliyonayo.
Kwa kulitambua hilo, Namungo kazi inaanza rasmi wakati huu na mechi ya marudio kimataifa itatoa picha ya kile ambacho kinahitajika na timu pamoja na mashabiki.
Wachezaji wakati huu ni wenu kutimiza yale ambayo mlikuwa mnaambiwa na mwalimu kwenye mazoezi kwa vitendo.
Makosa yaliyopita mwaka 2020 yawekwe kando kwa kuwa sasa tupo 2021 na mapambano yanaanza upya kabisa tena kwa kasi kubwa ya kufuata mafanikio.
Ule ushindi wa mabao 2-0 mlioupata nyumbani muda wake umeisha kwa kuwa mkipoteza mchezo wenu wa marudio na safari ya kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania itakuwa imegota kwenye kikomo.
Ukiachana na Namungo ambao walianza kwa kushinda mchezo wao wa mwaka uliopita wapo pia wawakilishi kwenye Ligi ya Mabingwa ambao ni Simba.
Namungo wanaipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho na ikiwa watatolewa safari yao itakuwa imefika mwisho.
Leo Januari 5, Namungo itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi mbele ya El Hilal Obeid ya Sudan mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Simba huku kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakitolewa na safari yao ya kutinga hatua ya makundi itakuwa imeyeyuka jumla wataangukia kwenye Kombe la Shirikisho.
Kazi inaanza upya kwani kupoteza kwa kufungwa na FC Platinum bao 1-0 sio mwisho wa safari hiyo ilikuwa ni 2020 na sasa tupo 2021.
Kikubwa ni kwamba kampeni ya Simba ya War In Dar ni nzuri ikiwa itajengwa katika misingi ya nidhamu na upambanaji bila kutegemea rekodi za Uwanja wa Mkapa.
Ipo wazi kwamba rekodi zimewekwa ili zivunjwe hivyo ikiwa Simba inatamba kwamba haijawahi kufungwa Uwanja wa Mkapa, ikibweteka itapoteza mbele ya FC Platinum.
Ubaya ni kwamba ikiwa itafungwa ama italazimisha sare habari ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika itakuwa imefika ukingoni. Inachotakiwa kufanya ni kupambana kusaka ushindi.
Mapambano yanaanza upya kwa wawakilishi wetu kimataifa na kila kitu kinawezekana, mbinu ziwe za 2021 na zisiwe zile za 2020.