CLATOUS Chama, nyota wa kikosi cha Simba mwenye tuzo ya mchezaji bora kwa msimu wa 2019/20 ndani ya Ligi Kuu Bara inatajwa kuwa itakua ngumu kwake kubaki ndani ya kikosi hicho mkataba wake utakapomeguka.
Nyota huyo alikuwa chaguo la kwanza la aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Sven Vandenbroeck ambaye amesepa ardhi ya Bongo kuelekea nchini Ubelgiji baada ya kueleza kuwa ni masuala ya familia.
Sven aliweka wazi kuwa anaamini itakuwa ngumu kwa nyota huyo kubaki ndani ya Simba kwa kuwa amekuwa akionyesha uwezo mkubwa na kujituma jambo linalomuongezea thamani.
“Kwa namna ambavyo ninaona kwa Chama kubaki ndani ya Simba itakuwa ngumu kwa kuwa anaonyesha uwezo mkubwa ndani ya uwanja.
“Ukifanya vizuri ni rahisi kuwavutia wengine na unajua kwamba mchezaji ni biashara jukumu la kubaki ama kuondoka ni lake mwenyewe anaweza kwenda popote anapotaka,” alisema wakati alipozungumza na Spoti Xtra.
Chama amekuwa na mchango mkubwa ndani ya Simba kwa msimu wa 2020/21 katika kutimiza majukumu yake ya kuipeleka timu hiyo hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbele ya FC Platinum kwenye mchezo wa marudio uliochezwa Uwanja wa Mkapa alikuwa ni mchezaji wa namba moja kwenye mechi hiyo kwa kuwa alihusika kwenye mabao yote manne yaliyofungwa.
Bao la kwanza ambalo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Erasto Nyoni alitoa pasi kuelekea kwa Shomari Kapombe ambaye alidondoshwa nje kidogo ya 18 na mwamuzi kutafsiri penalti.
Bao la pili lililofungwa na Shomari Kapombe baada ya kipa wa FC Platinum kuutema mpira wa Rarry Bwalya alikuwa mmoja ya waliokuwa kwenye mwendo wa kugongeana pasi na pia bao la tatu la John Bocco, pasi ya Bwalya ilitoka mguuni mwa Chama.
Msumari wake wa mwisho yeye mwenyewe alipachika kwa penalti baada ya yeye mwenyewe kuchezewa penalti hiyo na kufanya timu yake ishinde mabao 4-0 na kutinga hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-1.
Jumla ana mabao mawili ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa bao la kwanza alifunga dhidi ya Plateau United, Uwanja wa New Jos baada ya kupewa pasi na mshikaji wake Luis Miquissone.
Nyota huyo anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga ambapo mkataba wake unatarajiwa kufika ukingoni msimu ujao huku stori yake ya kusaini mkataba mpya ikitajwa kuwa haijakamilika kutokana na dau ambalo analihitaji.
Pia wapinzani wao FC Platinum wanatajwa kuvutiwa na uwezo wa nyota huyo.