UONGOZI wa Simba umesema kuwa kwa sasa mchakato wa kumpata mrithi wa Sven Vandenbroeck unaendelea hivyo ni suala la mashabiki kuwa na subira.
Vandenbroeck alisepa ndani ya kikosi cha Simba baada ya kukiongoza kikosi hicho kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Januari 6, Simba ilishinda mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum na kufanya itinge hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 4-1 kwa sababu mchezo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe na mchezo wa pili ikashinda.
Barbara Gonzalez, Mtendaji Mkuu wa Simba, (CEO) amesema kuwa wamepokeza CV zaidi ya 65 na mpaka wakati huu tayari wamezifanyia mchujo baadhi ya CV hizo ili kupata kocha ambaye wanamhitaji.
“Kwa sasa bado mchakato wa kumsaka kocha ndani ya Simba unaendelea, mashabiki wasiwe na presha kila kitu kinakwenda sawa kwa kuwa wengi wametuma CV ili kupata nafasi ya kukinoa kikosi cha Simba.
“Nimegunuda kwamba Simba ni timu kubwa na wengi wanaipenda hivyo hatuwezi kukosa mtu wa kuifundisha timu yetu kwa sasa hivyo ni suala la kusubiri na kuona,” amesema.
Miongoni mwa makocha amabao wanatajwa kuibukia ndani ya Simba ni pamoja na Kocha Mkuu wa AS Vita, Florent Ibenge ambaye anapewa chapuo la kubeba mikoba ya Sven.