MTAMBO wa mabao ndani ya Klabu ya Yanga unatarajiwa kutua kesho ili kuungana na wachezaji wenzake kambini kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kurejea Februari 13.
Michael Sarpong alikwea pipa kueleka Ghana baada ya kumaliza kazi ya kusaka Kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar, Januari 13.
Yanga iliweza kutwaa taji la kwanza ndani ya 2021 kwa kuwafunga watani zao wa jadi, Simba kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kukamilika bila kufungana.
Mtambo huo wa mabao ndani ya Yanga pia ulikuwepo kwenye kikosi cha kwanza kilichoanza Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar.
Ndani ya Ligi Kuu Bara, Sarpong ametupia jumla ya mabao manne idadi ambayo ni sawa na mshikaji wake Yacouba Songne pamoja na Deus Kaseke.
Katika mabao hayo anaingia kwenye rekodi ya kumtungua kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula kwenye Dar, Dabi iliyokamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Uwanja wa Mkapa.
Nyota huyo ambaye amesaini dili la miaka miwili anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao hawataongezewa mkataba ikiwa kiwango chake kitashindwa kuimarika.
Kaimu Katibu wa Yanga, Haji Mfikirwa amesema:”Sarpong hivi sasa amerudi nchini kwao Ghana kwa ruhusa maalumu ambayo amepewa na uongozi na anatarajiwa kurejea Januari 25,” .