SIMBA ndio wawakilishi pekee wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ratiba ambayo Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) liliyotoa mapema ni kwamba Wekundu wa Msimbazi watakutana na timu tatu kutoka mataifa matatu tofauti.
Simba imepangwa kundi moja na AS Vita ya DR Congo, El Merreikh ya Sudan na Al Ahly ya Misri ambapo timu mbili pekee zitatakiwa kupambana ili kuvuka hatua hiyo na kwenda hatua ya robo fainali ya ligi hiyo.
Hata hivyo, katika uwepo wa ratiba hiyo, Mwanaspotil inabaini kutakuwa na vita ya ndani kwa ndani tofauti tano ambazo Simba italazimika kupigana dhidi ya mtu mmojammoja au kama timu kulingana na maisha ya nyuma.
Simba vs As Vitta
Vita ya kwanza itakuwa ni ya marudiano ya kisasi kati ya Simba na AS Vita. Itakumbukwa misimu miwili iliyopita timu hizi mbili zilikutana katika hatua kama hii ambapo Vita ilishinda kwa kishindo katika mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani kwa mabao 5-0 kipigo ambacho kilichowaumiza wekundu hao.
Simba nao wakalipa kisasi wakishinda mchezo muhimu wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wakishinda kwa mabao 2-1, lakini ushindi huo ukaivusha Simba kwenda hatua ya robo fainali huku Wakongomani hao wakitupwa nje ya mashindano na sasa wanakutana huku Wekundu wa Msimbazi wakitaka kuendeleza ubabe wao wakati wenzao wakitaka kulipa kisasi.
Simba vs Al Ahly
Hapa napo kutakuwa na vita ya kisasi ni kama ilivyokuwa kwa AS Vita. Hii ni kwamba Al Ahly ilimchapa Simba mabao 5-0 katika mchezo huko kwao nchini Misri huku Simba ikionekana kuzidiwa karibu kila kitu na mabingwa hao wa kihistoria wenye rekodi bora ya mataji. Mchezo wa marudiano Simba ikaendeleza msimamo wao kwamba mgeni hashindi kwao wakaichapa Ahly bao 1-0 katika mchezo mgumu nyumbani ingawa timu hizo mbili baadaye ndizo zilizotinga hatua ya robo fainali na sasa watakutana tena kwa Simba kutaka kuweka sawa rekodi yao, pia Ahly wakitamani wasiharibiwe heshima ya kuwa klabu kubwa wakitaka kushinda mechi zote mbili.
Bwalya vs Simba
Al Ahly wataongozwa na mshambuliaji wao mpya Walter Bwalya aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Al Gounah ya nchini Misri, lakini Bwalya ana kisasi na Simba hawakumuacha salama mara ya mwisho alipokutana nao.
Alipokuwa Nkana ya Zambia, Bwalya akiwa nahodha wa timu hiyo walicheza mechi mbili na Simba – ya kwanza Nkana wakiwa nyumbani walishinda mabao 2-1 kisha wakacheza mchezo wa marudiano katika Uwanja wa Mkapa ambapo bao lake liliitanguliza Nkana lakini baadaye Simba wakabadilika.
Simba ilirudisha bao hilo na kuongeza mengine matatu, lakini bao ambalo halitasahaulika kwa Bwalya ni lile la tatu likifungwa kiufundi na Clatous Chama katika dakika za majeruhi na kuifanya Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa huku Nkana ikirudi Kombe la Shirikisho ambapo Bwalya hatasahau umafia huu wa Simba akitaka kulipa kisasi.
Gomes vs El Merreikh
Simba sasa ipo chini ya kocha Didier Gomes raia wa Ufaransa lakini katika hatua mbaya sana inayotia hasira ni kwamba kocha huyo kabla ya kutua Simba alifanya maamuzi magumu akivunja mkataba na klabu yake ya Al Merreikh ya Sudan kisha akatua haraka nchini Tanzania kusaini mkataba wa miaka miwili na Simba.
Wakati Gomes akitua Simba aliiwezesha Al Merreikh kutinga hatua ya makundi pia, ratiba ilipotoka tayari Waarabu hao walikuwa wamepangwa na Simba kundi moja na hapo Al Merreikh hawatataka kumpa jeuri ya kusema kocha wao huyo wa zamani lakini Simba itaringia uwepo wa mtaalamu huyo wakijua kwamba wana mtu muhimu katika benchi lao ambaye anawajua vyema wapinzani wao.
Tshishimbi vs Simba
Ndani ya kikosi cha AS Vita katika hatua ya makundi watakuwa na kiungo wao, Pappy Tshishimbi ambaye ataanza kuitumikia timu hiyo katika mechi za hatua ya makundi lakini Simba na Tshishimbi pia watakuwa na vita yao tofauti. Kabla ya kutua Vita, Tshishimbi alitokea Yanga ambako alikuwa nahodha na akiwa huko mara ya mwisho alipokutana na Simba wakachukua mabao 4-1 katika mchezo ambao unawezekana ulichangia Yanga kutomuongezea mkataba kiungo huyo na sasa watakutana huku Tshishimbi akitaka kulipa kisasi na Simba wakitaka kumuonyesha wao wako sawa.
Msikie Tshishimbi
Kuhusu mchezo huo, Tshishimbi anasema hawezi kuukamia sana, lakini kwa timu waliyonayo ana imani AS Vita itakuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa hawatakiwi kufanya makosa mara mbili.
“Najua Simba wananijua lakini niseme furaha yangu ni kurejea hapo nikiwa na timu ambayo naamini sasa ina kikosi imara na wana malengo makubwa katika mashindano haya ya Afrika,” alisema Tshishimbi. “Simba wananijua na mimi nawajua ni timu nzuri lakini naamini Vitta ina wachezaji bora zaidi ambao wanajua kuamua mechi kubwa kama hizi, nitafurahi kama Vitta ikishinda na sidhani kama itakuwa rahisi kufanya makosa hayo mara mbili naamini itakuwa mechi ngumu.”