Home Yanga SC A-Z JINSI YANGA WALIVYOTUMIA ZAIDI YA MILIONI 550 KUSHINDA MECHI ZA LIGI...

A-Z JINSI YANGA WALIVYOTUMIA ZAIDI YA MILIONI 550 KUSHINDA MECHI ZA LIGI KUU


KUANZIA ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, Machi 8, 2020, Yanga ndio timu ambayo imecheza idadi kubwa ya mechi bila kupoteza katika Ligi Kuu na mashindano mengine.

Timu hiyo imepoteza jumla ya mechi mbili tu kati ya 38 ilizocheza katika Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Shirikisho la Azam.

Katika mechi hizo 38, imetoka sare kwenye mechi 13 na na kuibuka na ushindi katika jumla ya mechi 23 huku ikitwaa taji la Mapinduzi mwaka huu na kumaliza katika nafasi ta pili kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.

Lakini mafanikio hayo hayajaja kirahisi na badala yake timu hiyo imetumia fungu la zaidi ya shilingi 550 milioni kama bonasi ya kuwajaza morali wachezaji wa kikosi hicho hadi kikamudu kupoteza idadi ndogo zaidi ya mechi kulinganisha na wengine.

Katika kitita hicho cha fedha ambacho kimetumika na Yanga kama bonasi kwa wachezaji wake, fungu kubwa la takribani Sh 500 walitumia katika mechi mbili tu ambazo ni dhidi ya Simba katika Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi.

Neema kwa wachezaji wa Yanga ilianza kuwaangukia katika mechi waliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba ambayo baada ya hapo walipewa bonasi ya Shilingi 200 kutokwa kwa mdhamini wa klabu hiyo, kampuni ya GSM.

Kiasi hicho cha fedha kinaonekana kilitokana na ukubwa na thamani ya mechi hiyo kwani kwa utaratibu wa kawaida katika msimu uliopita, GSM walikuwa wakitoa kitita cha Sh 10 milioni kwa timu pindi ilipokuwa ikishinda kila mchezo.

Baada ya kuvuna Sh 200 milioni kwa kuiangusha Simba, nyota wa Yanga walikuja kupata takribani Sh 50 milioni baada ya kupata ushindi katika mechi tano zilizofuata za Ligi Kuu hadi msimu ulipomalizika ambapo katika kil mechi waliyoshinda walipata Sh 10 kama utaratibu wa kawaida uliowekwa katika msimu huu.

Hata hivyo licha ya Yanga kuweka utaratibu mpya wa bonasi msimu huu tofauti na ule wa msimu uliopita ambapo timu ilikuwa ikipatiwa Sh 10 milioni kwa kila mechi wanayoshinda.

SOMA NA HII  ISHU YA FARID MUSSA KUTEMWA YANGA IPO HIVI

Hata hivyo, Yanga kupitia GSM waliibuka kivingine Januari 13 mwaka huu pale walipotwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kuwachapa Simba kwa mikwaju ya penati 4-3 baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika dakika 90 za fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuwapa wachezaji wa timu hiyo kitita cha Sh 300 milioni kama zawadi kwa kutwaa ubingwa huo huku wakiwa wamewafunga watani wao wa jadi.

Lakini pia huenda fungu hilo likawa kubwa zaidi kwani na msimu huu wamekuwa wakitoa bonasi katika mechi za ligi ingawa kiwango cha fedha wanachotoa hakijawekwa wazi tofauti na msimu uliopita.

Ofisa uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alisema kuwa bonasi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri kwa timu hiyo katika mashindano wanayoshiriki.

“Mpira wa kisasa ili ufanikiwe unahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha hivyo lazima tuwe wakweli kwamba mdhamini wetu GSM amekuwa akijitolea sana kuhakikisha wachezaji na makocha wanaishi vizuri jambo linaloongeza morali na hamasa kwao.

Jambo la msingi kwa wanachama na mashabiki wa Yanga ni kuwaunga mkono wadhamini wetu kwa kununua bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu ili kuongeza mapato ya timu iweze kufanya vizuri zaidi,” alisema Nugaz

Nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisema kinachofanywa na uongozi wa Yanga na wadhamini wao kitaifanya Yanga iwe tishio zaidi.

“Sisi tulicheza soka kwa mapenzi lakini kwa sasa hali ni tofauti lakini wadhamini na viongozi wetu wanajitahidi kuwatimizia wachezaji mahitaji yao jambo ambalo linachangia wafanye vizuri.”