LICHA ya kusaini dili la miaka miwili ndani ya Klabu ya Simba inaelezwa kuwa mwamba Perfect Chikwende akili yake ipo Azam FC ila mwili upo Simba.
Nyota huyo ambaye amesaini dili hilo kwenye usajili wa dirisha dogo lililofungwa Januari 16 baada ya kufunguliwa Desemba 15 alikuwa anahitajika na Azam FC.
Dili lake ndani ya Azam FC lilikwamba baada ya kile ambacho mabosi wa timu hiyo walisema kuwa Kocha Mkuu, Geroge Lwandamina hakumhitaji ndani ya kikosi hicho.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa ingekuwa Azam FC wanahitaji saini yake ingekuwa ngumu winga huyo kuibukia ndani ya Simba
“Ipo wazi kwamba Chikwende anapenda kuwa ndani ya Azam FC ila hana chaguo kwa kuwa mwalimu alimkataa ila kama ingekuwa anahitaji saini yake asingekuwa Simba.
“Kama Azam FC tunahitaji mchezaji kutoka Zimbabwe, wengi ni rahisi kumpata kwa sababu wengi wanaitambua Azam FC kwa uzuri na wanapenda kucheza hapa hivyo hatukushindwa kumsajili.
“Sisi tunamskiliza mwalimu anasema nini akishasema huyu mchezaji hapana basi tunamuacha hatuendelei kumfuatilia kabisa,” .
Chikwende alitua ndani ya Simba akitokea Klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe ambalo ilicheza na Simba kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Walipokutana ndani ya Uwanja wa Taifa ya Zimbabwe, FC Platinum walishinda bao 1-0 ambalo lilifungwa na Chikwende mwenye ila ngoma ilizimwa Uwanja wa Mkapa kwa Simba kushinda mabao 4-0 na kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.