DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amepata majembe 7 ya kazi ndani ya kikosi hicho kupitia kwenye mechi mbili za Simba Super Cup iliyofanyika Dar na timu hiyo kuweza kutwaa taji hilo ikiwa na pointi nne.
Baada ya kurithi mikoba ya Sven Vandenbroeck ambaye alibwaga manyanga Januari 7, na kuibukia Morocco kwenye Klabu ya FAR Rabat, aliweza kuiongoza timu kwenye mechi mbili huku nyota 7 wakipata zali kwenye mechi hizo kuanza kikosi cha kwanza.
Kwenye mechi mbili ambazo ilikuwa ni dhidi ya Al Hilal ya Sudan na TP Mazembe ya Congo langoni alimuamini Beno Kakolanya ambaye alicheza mechi zote mbili na kuyeyusha dakika 180, amefungwa bao moja ilikuwa mbele ya Al Hilal na ana tuzo ya kipa bora wa mashindano.
David Kameta, alikuwa amebeba mikoba ya Shomari Kapombe aliyeyusha dakika zote 180 aliweza kuonyesha umwamba huku akiwa na zawadi ya kadi moja ya njano ilikuwa mbele ya TP Mazembe.
Mohamed Hussein, beki huyu mzawa aliyeyusha dakika zote 180 ndani ya uwanja, Joash Onyango aliaminiwa na kuyeyusha dakika zote 180. Ingizo jipya Thadeo Lwanga, kiungo huyu mkabaji mbele ya Al Hilal alitumia dakika 80 na mbele ya TP Mazembe alitumia dakika 85 hivyo jumla ametumia dakika 165.
Larry Bwalya mchezaji bora wa mashindano hayo mbele ya TP Mazembe alitumia dakika 75 huku 90 akiyeyusha mbele ya Al Hilal jumla ametumia dakika 165. Clatous Chama mbele ya Al Hilal alitumia dakika 74 na mbele ya TP Mazembe alitumia dakika 85 jumla ametumia dakika 159.