INGIZO jipya ndani ya kikosi cha Yanga,Fiston Abdoul Razack akiwa amepewa dili la miezi sita aliweza kuweka rekodi yake ndani ya kikosi hicho kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya African Sports ya Tanga kwa kutumia dakika 10 za awali bila kugusa mpira.
Ikiwa ni mchezo wake wa kwanza kwenye ardhi ya Bongo, wapinzani wake African Sports walimuweka kwenye ulinzi mkali ambapo mipira yote aliyokuwa anapewa kupitia kwa mshambuliaji Wazir Junior, Haruna Niyonzima na Tuisila Kisinda ilikuwa inakutana na ukuta matata.
Aliweza kugusa mpira na kutoa pasi makini dakika ya 11 baada ya Niyonzima kutumia uzoefu kukwepa mitego ya mabeki ambao walikuwa wakiwazuia Yanga kupenya ngome yao.
Kaze alimpa dakika 78, ambapo katika dakika hizo aliweza kuonekana na utulivu katika umiliki wa mpira na kuwakimbia wapinzani huku akionekana kuwa na uchu wa kufunga.
Anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyeotea mara nyingi akiwa amefanya hivyo mara nne kwa kipindi cha kwanza na alipiga jumla ya pasi 15, alikokota mpira mara tatu huku akicheza jumla ya faulo mbili.
Kaze amesema kuwa kwa muda ambao alimpa nyota huyo anaamini kwamba atakuwa imara na kurejea kwenye ubora wake ambao anao ndani ya uwanja.
“Fiston ni mchezaji mzuri na anauwezo wa kufanya kazi kwa muda ambao amefanya kazi uwanjani sio wa kubeza nina amini kadri siku zinavyokwenda atakuwa imara bila shaka yoyote,” amesema Kaze.