MATHIAS Lule, Kocha Mkuu wa Mbeya City amesema kuwa hawezi kubadili maamuzi ya mwamuzi kuhusu bao walilofungwa jana na Yanga ambalo lilionekana kulalamikiwa na wachezaji wa Mbeya City.
Mbeya City jana ilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 na Yanga kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.
Bao la Yanga lilifungwa na Deus Kaseke dakika ya 84 ambapo ilionekana kwamba mpira huo ulikuwa umeokolewa na beki wa Mbeya City kabla ya kujaa nyavuni jambo ambalo liliwafanya wachezaji wa Mbeya City kumlalamikia mwamuzi huku mlinda mlango, Harn Mandanda akionyeshwa kadi ya njano.
Mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Yanga ilisepa na pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 ila jana iliweza kugawana pointi na Mbeya, jumla kwenye pointi sita, Yanga imesepa na nne huku Mbeya ikisepa na pointi moja.
Lule amesema kuwa kupata pointi mbele ya vinara wa ligi sio jambo dogo hivyo anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana.
“Mwanzo tulikosea kwenye zile dakika za mwanzo hasa kwa wachezaji kushindwa kufuata maelekezo ila baadaye waliweza kurejea kwenye mchezo.
“Kuhusu bao ambalo tumefungwa siwezi kulizungumzia kwa kuwa mwamuzi akishaamua kuwa ni bao huwezi kubadili maamuzi yake kwetu sisi kwa kuwa tumepata pointi moja tunajipanga kwa ajili ya mechi zijazo,”.