KILA kitu kinakwenda kwa namna ambavyo unapanga na kupambana ili kuona mwisho wa siku unapata matokeo ya kile ambacho unakihitaji.
Ila inabidi ukumbuke kufanya kazi kwa juhudi ni jukumu lako ila suala la mafanikio muachie Mungu kwa kuwa yeye anajua namna ya kugawa riziki.
Hapo ndipo ambapo imekuwa ni mtihani kwa baadhi ya wachezaji linapofika suala la kukubali matokeo ndani ya uwanja.
Hali hiyo pia imeambukizwa mpaka kwa mashabiki nao wana kasumba ya kugoma kukubali matokeo ndani ya uwanja baada ya dakika 90.
Tatizo limezidi kuwa kubwa si kwa Yanga, Simba,KMC Lipuli mpaka Njombe Mji unaambiwa hakuna ambaye anakubali matokeo ya aina yoyote kwa pande hizi mbili.
Nakumbuka Simba ilishinda mabao 4-0 dhidi ya JKT Tanzania, baada ya dakika 90 kuisha mashabiki kama kawaida walianza kusikitika kweli na kusema ilikuwa mtu apigwe nane, sema wachezaji walijisahau na kuanza kupiga pasi nyingi.
Weka kando hiyo Simba ilipopoteza mechi mbili mfululizo mbele ya Tanzania Prisons kisha ikapoteza mbele ya Ruvu Shooting, maneno. Hakuna shabiki ambaye alikubali matokeo.
Wakaanza Clatous Chama hayupo sasa timu inarukaruka tu, mfumo wa mwalimu mbovu yaani ilimradi tu hakuna anayekubali matokeo.
Njoo kwa ndugu zetu KMC wazee wa pira spana, walipokutana na wale Wajelajela, Tanzania Prisons na kupoteza kwa kufungwa mabao 2-1, unaambiwa matokeo hayo yalisababishwa na mvua kunyesha jambo lililowafanya wasiwe na namna wachezaji kusaka ushindi.
Sare ya bao 1-1 waliyopata Yanga mbele ya Mbeya City,wachezaji walivimba kila mmoja anataka kumvamia mwamuzi sasa sijui walitaka kumfanya nini wanajua wenyewe.
Lamine Moro ilibidi abadilishe majukumu na kuwa mlinzi wa mwamuzi, mashabiki nao sasa kama kawaida kwao kurusha makopo ni kawaida. Muda wa ugomvi uwanjani umekwisha kwa sasa.
Matokeo yake ni kwamba vurugu hizo zimewafanya Yanga watozwe faini ya laki tano ambayo haikuwa na ulazima wa kufanya hivyo kwa namna yoyote ile, mpira ni ndani ya uwanja.
Hatukatai kwamba ni lazima kuongea pale matokeo yanapokuwa mabovu hata mazuri ila ni muhimu kuwa na mipaka na nidhamu katika kuzungumza na kuchukua sheria mikononi.
Kuna shabiki mwingine ameweka wazi kwamba anaweza kumdhuru mwamuzi, kisa sare. Naona hii sio sawa, mpira sio vita mpira ni burudani.
Zipo sababu ambazo zinasababisha timu ishindwe kupata matokeo, ubovu wa miundombinu ni sababu hasa kwa mazingira ya Tanzania, viwanja bora vinahesabika.
Ukianza na kwa Mkapa, Azam Complex,Uhuru, Kaitaba sasa hivyo vingine taratibu sehemu ya kuchezea haina ubora hivyo iwe somo kwa wamiliki wa timu kugandamizia mpango wa Azam FC kwa kumiliki uwanja wao wa kisasa.
Masuala ya kuleta vurugu na makelele baada ya mpira sio sawa kikubwa ni kuwa watulivu na kushangilia bila kuogopa. Wachezaji kazi yenu iwe moja kusaka ushindi ikitokea mkapata sare, mkapoteza ama mkashinda sawa.
Muhimu kwa kila timu kuweza kuwa na maandalizi mazuri, mzunguko wa pili una ushindani mkubwa na kila timu inahitaji ushindi.
Ikiwa kila siku unataka timu yako ishinde sasa timu ya nani unataka ishindwe na kwa nini?