SARE tatu mfululizo ilizopata Yanga Ligi Kuu kabla ya mchezo wa jana zimewashtua na kuwachanganya mashabiki wa timu hiyo wakiona ni kama wamekabidhi mbio za ubingwa kwa watani wao Simba, lakini Mshauri wa klabu hiyo, Senzo Masingiza amewatuliza mashabiki hao.
Wasiwasi huo wa mashabiki wa Yanga ukakolea zaidi na mbio za watani wao waliokuwa nyuma yao wakiendelea kushinda viporo vyao, lakini Senzo aliyefanya kazi katika klabu zote mbili hizo kwa vipindi tofauti amewaambia mashabiki hao watulie kwani msimu huu lazima wabebe ndoo.
Akizungumza na gazetila Mwanaspoti, Senzo aliwaambia wanachama na mashabiki wa Yanga haijatoka katika mbio za ubingwa kama wengi wanavyofikiri na kudai kama walikuwa wakitembea na wameteleza au kujikwaa ingawa hawakufika chini.
“Kilichotokea kwetu ni kama tumeteleza au kujikwaa na hatua hiyo hatukifika kushika chini bado tunaendelea na safari, sioni kabisa kama Yanga imetoka katika mbio za ubingwa, japo kilichotutokea hakikuwa kizuri,” alisema Senzo ambaye ni msimu huu alihama kutoka Simba kisha kutua Yanga katika muvi ambayo iliwashtua wengi.
“Yanga bado iko imara na tunataka mataji tumepoteza pointi sita katika mechi tatu hatua hii inaweza kutokea kwa timu yoyote kwa kuwa ligi bado sana kufikia hatua ya kukata tamaa. Wanachama lazima watulie na kuiunga mkono timu yao, kwani nafasi ipo ya kurejesha ubingwa Jangwani.”
Senzo alisema wao kama uongozi wanajua wapi kulikuwa na shida na bahati nzuri kwao hakuna mgogoro wowote na karibu kila kitu kipo sawa na watarejea na nguvu kubwa kuhakikisha wanatuliza presha ya mashabiki wao.
Alisema jambo zuri kwao ni kwamba hatua ya kupoteza pointi hizo imewaumiza hata wachezaji na wamewaahidi kwamba watapambana kuhakikisha ushindi unarudi hali kadhalika makocha nao wameonyesha juhudi kubwa katika kuondoa changamoto hizo.
“Tunajua mashabiki na wanachama wetu waliumia na hiki ambacho kimetokea ni kama sisi viongozi na hata makocha na wachezaji, sisi ni timu moja na ndio maana tukaitwa timu ya wananchi tunapoteza pamoja na tunashinda pamoja.
“Wachezaji wameahidi mambo makubwa wanataka kurudi kwa nguvu na sisi kama uongozi tuko pamoja na nao kwa kuwa hakuna madai yoyote kwao haya ni matokeo ya soka kuna wakati unateleza ligi bado tuna nafasi kubwa ya kubadilisha mambo.
“Mashabiki na wanachama wetu wapendwa wanatakiwa kuendelea kuwa wamoja na kuendelea kuipigania timu yao kokote inapocheza hii ndio maana halisi ya timu ya wananchi kama uongozi tunaona bado tuna nafasi kilichotokea kwetu kinaweza kutokea kwa timu nyingine yoyote.”