UONGOZI wa Simba umesema kuwa licha ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi safari bado inaendelea.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez ameweka wazi kuwa malengo ya Simba ni kutwaa ubingwa wa Afrika.
Ikiwa Uwanja wa Mkapa leo Februari 23 iliweza kucheza kwa nidhamu ndani ya dakika 90 mbele ya washindi wa tatu wa Klabu Bingwa Duniani, Al Ahly ya Misri.
Bao pekee la ushindi kwa Simba lilijazwa kimiani na nyota wao Luis Miquissone ambaye alitajwa jana na Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Misomane ambaye aliweka wazi kwamba ni moja ya mchezaji ambaye anamtambua na uwezo wake ni mkubwa.
Luis alipachika bao hilo dakika ya 30 akiwa nje ya 18 kwa shuti kali ambalo lilimshinda mlinda mlango wa Al Ahly.
Ushindi huo unaifanya Simba kurejea pale ambapo walianza awali kwenye nafasi ya kwanza katika kundi A baada ya kufikisha jumla ya pointi sita.
AS Vita wanakuwa nafasi ya pili na pointi zao tatu sawa na Al Ahly ambayo ipo nafasi ya tatu na ina pointi tatu huku Al-Merriekh ikiwa nafasi ya nne na haijakusanya pointi.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara amesema:-Pongezi kubwa kwa wachezaji wote pamoja na benchi la ufundi. Endelea kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu vijana wetu.Tuendeleze mshikamano wetu ili tufikie lengo letu la kuwa mabingwa wa Afrika, Insha’Allah! Safari inaendelea,” ,