KATIKA kuhakikisha kikosi chake kinafanya vema kwenye Kombe la FA, Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, amesema haitaidharau timu yoyote atakayokutana nayo.
Yanga hivi sasa ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa Kombe la FA utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam dhidi ya Kengold ya Mbeya inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kaze alisema hawaifahamu vizuri Kengold, hivyo wataingia uwanjani wakiwa na kikosi kamili na kikubwa ni kuwafunga ili kusonga mbele katika michuano hiyo.
Kaze alisema kuwa hivi sasa kila mchezo wanauchukulia kama fainali bila ya kuidharau timu yoyote kwani wanataka kutimiza malengo yao msimu huu ambayo ni kubeba ubingwa wa ligi na Kombe la FA.
“Kikosi changu kitaingia tofauti katika mchezo wa mzunguko wa nne wa Kombe la FA dhidi ya Kengold ili kuhakikishia tunapata ushindi mnono na kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
“Tumepanga kuingia uwanjani katika mchezo huu kama fainali kutokana na umuhimu mkubwa wa pambano hilo kwa lengo la kuvuka katika hatua hii kwenda nyingine.“Hivyo ni lazima tushinde bila ya kuwadharau wapinzani wetu, nimepanga kutumia wachezaji wangu wote muhimu kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Kaze.