Home Yanga SC YANGA YATINGA 16 BORA, NGUMI YAMPONZA MUANGOLA ALIMWA KADI NYEKUNDU

YANGA YATINGA 16 BORA, NGUMI YAMPONZA MUANGOLA ALIMWA KADI NYEKUNDU


 LICHA ya kumaliza dakika 90 wakiwa pungufu, leo Februari 27, Uwanja wa Uhuru kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Ken Gold bado waliweza kulinda ushindi wao wa bao 1-0 walilolipata.

Ni Fiston Abdulazack, ingizo jipya ndani ya Yanga ambaye alipachika bao la ushindi dakika ya 40 kwa mkwaju wa penalti uliomshinda kipa wa Ken Gold, Adam John.

Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha pili licha ya nyota wa Ken Gold kupambana kuweza kuweka usawa kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Jitihada zao zilikwama kwenye mikono ya kipa Faroukh Shikalo ambaye alianza kikosi cha kwanza.

Dakika ya 80 kiungo Carlos Carlinhos, raia wa Angola alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Ken Gold jambo lililopelekea mwamuzi kumuonyesha kadi hiyo.

Inakuwa ni kadi ya kwanza kwa nyota huyo wa Yanga mwenye mabao matatu ndani ya Ligi Kuu Bara na aliingia akitoka benchi kuchukua nafasi ya mshambuliaji Ditram Nchimbi.

Ushindi huo unaifanya Yanga itinge hatua ya 16 bora huku ikisubiri mshindi wa mchezo wa kesho kati ya Sahare All Stars ama Polisi Tanzania kwenye hatua ya 16 bora na timu hizo zinatarajiwa kumenyana kesho.

Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema kuwa wachezaji walipambana kusaka ushindi na wamefanikiwa lengo lao jambo ambalo linawapasa pongezi.

SOMA NA HII  KAZE AIPA NAFASI SIMBA KUTUSUA KIMATAIFA